Rudi miaka miwili iliyopita kisha hesabu mpaka mwaka 2006, Ali Kiba alikuwa mwanamuziki anayeogopwa mno. Wanamuziki wenzake walimchukulia kama kioo cha mafanikio. Alistahili kutokana na uwezo wake lakini alichokosea ni kwamba hakukaza ili kufika mbali.
Haikuwa kuogopwa tu na wanamuziki wenzake, bali kwa mashabiki pia Ali Kiba ni kipenzi chao mpaka leo. Alikuwa na mtaji mkubwa mno wa kumuwezesha kutengeneza fedha nyingi kupitia muziki wake, vilevile kutamba kimataifa.
Alishafanya kazi na Mfalme wa R&B duniani, R. Kelly katika ‘project’ ya One8 (Hands Across the World) ambayo iliwakutanisha mastaa wakubwa barani Afrika. Ulikuwa mtaji mkubwa sana kwake na hakutakiwa kurudi chini katika ‘levo’ za kinyumbani, alishakuwa wa kimataifa.
Hapa namlaumu Ali Kiba mwenyewe lakini zaidi menejimenti yake. Frank Mgoyo na Seven kama mameneja wake, hawakufanya kazi inavyotakiwa kuhakikisha wanazidi kumuuza mwanamuziki wao kila kona ya Bara la Afrika na dunia kwa jumla.
Muziki ni kazi ya matangazo, Tanzania tusingewajua P Square kama menejimenti yake isingewajibika kuwatangaza katika kiwango ambacho Afrika nzima ikakubali kwamba mapacha hao wanafanya muziki mzuri.
Ni kweli kuwa Ali Kiba alikuwa anafanya maonesho mengi nje ya nchi kuliko ndani lakini shoo hizo mara nyingi hazina mvuto kwa sababu kule anakwenda kutumbuiza watu wachache. Tumbuizo la idadi ndogo ya watu hushusha thamani ya mwanamuziki.
Laiti wangemtengenezea video nzuri zinazomuonesha Ali Kiba ‘akipafom’ kwenye maelfu ya Watanzania kisha kuzisambaza mitandaoni na katika kona mbalimbali Afrika, hapo mapromota wa nchi nyingine wangejua kumbe kuna kichwa kinachoweza kuvuta maelfu ya watu na kutengeneza fedha. Hawakufanya hivyo!
Februari 26, 2012, Ali Kiba alifanya shoo kubwa sana Dar Live na kuhudhuriwa na maelfu ya watazamaji. Kwa menejimenti makini, walipaswa kuwepo siku hiyo na kurekodi video za ‘promo’, hawakuwepo. Kuanzia hapo nikatambua kwamba Ali Kiba hana menejimenti sahihi.
Ali Kiba ni fundi sana wa kuimba, ubora wake unaishia katika ‘audio’ ambazo pia hazitangazwi inavyotakiwa. Menejimenti yake haikuwekeza katika video kuhakikisha nyimbo zake zinapigwa kwenye vituo vikubwa vya televisheni barani Afrika na duniani.
Channel 0 wangempa tuzo Ali Kiba kwa kazi ipi ambayo imepata nafasi kubwa katika televisheni yao? MTV wanamtambuaje ikiwa kazi zake hawajazipiga? Huwezi kumtengenezea msanii wako mazingira ya ‘kilokoloko’ halafu utarajie avume kimataifa. Kwa uchawi gani?
Agosti 9, mwaka huu, wakati nampeleka Yemi Alade Airport, akirejea kwao baada ya kumaliza kufanya onesho lake katika Tamasha la Usiku wa Matumaini, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kwenye gari ulisikika wimbo “Mwana” wa Ali Kiba.
Akaniambia wimbo mzuri, nikamwambia hiyo ndiyo Bongo Flava, akaniuliza mwanamuziki gani ameimba nikamtajia Ali Kiba, akaniambia hamjui kabisa licha ya kumfafanulia kuwa alikuwepo kwenye project ya One8 na aliimba Hands Across the World na 2Face, Fally Ipupa, Mr. Flavor, R. Kelly na mastaa wengine.
Katika maongezi akaniambia Diamond ni mwanamuziki mkubwa kwa sababu kwao Nigeria anajulikana. Akaniuliza kwa Tanzania kati ya Ali KIba na Diamond, nikamjibu wote ni wanamuziki wazuri, kazi zao zinakubalika sana Tanzania.
Nikamfafanulia kwamba Ali Kiba ni mwanamuziki mkubwa lakini Diamond anakua kwa kasi na anapaa kimataifa. Akaelewa!
Mwaka 2012, Diamond aliwahi kunishawishi mara kadhaa ili kampuni yetu iandae mpambano kati yake na Ali Kiba. Alijua huyo yupo juu na aliamini kwamba endapo hilo litafanikiwa angepaa. Haikuwa rahisi kwa Kiba. Alikataa na niliona sahihi kukataa.
Kushindwa kwake kujituma kutafuta njia za kulifikia soko la kimataifa, kutulia kana kwamba alipo ameshafika, ni mambo ambayo yamesababisha mafanikio aliyostahili kuyapata yeye, yamefikiwa na Diamond kabla yake. Pamoja na uzembe wa menejimenti yake, naye alipaswa kusoma alama za nyakati na kuchukua hatua.
Makosa ya Ali Kiba ndiyo hayohayo yaliyofanywa na Barnaba, anaimba vizuri lakini hafikii mahitaji ya soko la kimataifa. Matonya, MB Dog, Belle 9 na wengine wengi wapo mkumbo huo.
Nilishaeleza kuwa Diamond alitamani kupambanishwa na Ali Kiba. Tamasha la Usiku wa Matumaini 2012, tulimpambanisha na Dk. Jose Chameleone, alifurahi sana na hata aliposhindana na CMB Prezzo Julai 7, 2013, alikenua.
Desemba 25, 2012, tulipompambanisha na Ommy Dimpoz alinyong’onyea, alinilaumu kwamba kufaya vile ni kumshusha kwa sababu anataka awe anapambanishwa na wakubwa. Nilimwambia mbona iliwezekana kwa yeye na Chameleone, akakubali kwa shingo upande.
Utaona kiu yake, siku zote anataka kupanda juu. Huko nyuma kabla hata hajafanikiwa kurekodi wimbo na Davido, aliniambia anatamani siku moja akutanishwe jukwaa moja na P Square, kwamba kuanzia hapo atakuwa daraja lingine Afrika na duniani.
Aprili 29, 2012, baada ya kushuka naye kwenye helikopta katika ‘Shoo ya Helikopta’ Dar Live na kulakiwa na maelfu ya wakazi wa Mbagala, nilimwambia: “mdogo wangu unaona unavyokubalika? Kazi kwako.”
Alinijibu: “Kaka mimi siwezi kufanya uzembe, najua nilipotoka.”
Nilimkumbusha 20% alivyochezea nafasi alipokuwa juu kabisa ya kilele cha muziki Bongo. Akiwa kwenye kipindi kizuri cha kutengeneza pesa na kujitangaza kimataifa, akajifanya msela sana. Bahati ikamponyoka. Bahati bila juhudi ni kazi bure.
Ushauri wangu kwa wanamuziki ni kwamba kila mmoja awe na akili kama Diamond na asithubutu kuiga ubongo wa 20%, ni hasara kubwa.
ali kiba kilaza alilewa sifa za wabongo huyoo acha asote huyoo jera ya mziki daimond kaza butu tupige hela kama kawa kilaza alikiba unatofauti na mackmugani au ulijiimba mwenyewe hiyo nyimbo ..hahahaha
ReplyDelete