RAIS Jakaya Kikwete ameanza kazi rasmi baada ya afya yake kuimarika kufuatia upasuaji wa tezi dume aliofanyiwa mwezi uliopita nchini Marekani, huku akianza kushughulikia mambo ambayo yamekuwa yanasubiri maamuzi yake.
Kazi ya kwanza ilikuwa kumwapisha Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha, Daudi Felix Ntibenda katika shughuli fupi iliyofanyika jana asubuhi Ikulu, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Rais atakuwa anafanya kazi za ofisini na kwa muda mchache. Muda na kasi yake ya kufanya kazi vitaongezeka kwa kadri afya yake inavyozidi kuimarika.
Pamoja na kuanza kazi kwa kumwapisha Ntibenda, Rais Kikwete pia amepokea na kuanza kufanyia kazi maazimio manane ya Bunge kuhusu sakata la uchotaji fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow huku Watanzania wakihakikishiwa uamuzi utafanywa kwa kuzingatia misingi ya haki na uwazi.
Hayo yalithibitishwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, akisema Rais Kikwete ameagiza uchunguzi wa kina ufanyike kuhusu suala hilo kabla ya kupatiwa majibu hivi karibuni.
Balozi Sefue alitoa taarifa hiyo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kufahamu ni hatua gani na lini zitachukuliwa baada ya Rais kupokea maazimio hayo juzi.
Kwa mujibu wa Sefue, maazimio hayo ni mazuri na yamempatia nafasi na fursa nzuri Rais Kikwete ya kuendeleza uchunguzi wa kina kuhusu suala hilo jambo ambalo tayari ameanza kulitekeleza na litapatiwa majibu hivi karibuni.
“Napenda ifahamike kuwa hili ni suala kubwa, lakini mfumo mzima uko wazi, kila mhimili una wajibu wake, sasa mihimili ya Mahakama na Bunge imemaliza kazi zao sasa ni Serikali Kuu, tupeni nafasi tuyafanyie kazi haya maazimio, nawahakikishia haki itatendeka,” alisisitiza Sefue. Alisema kamwe Serikali haiwezi kudharau Bunge.
Alisema maazimio yote yaliyofikiwa na chombo hicho, yamechukuliwa kwa uzito mkubwa na ndiyo maana kila azimio litapitiwa na kufanyiwa kazi baada ya uchunguzi kukamilika.
Aidha, Sefue alisema kwa sasa vyombo vinavyochunguza suala hilo ni pamoja na vilivyofanya uchunguzi awali ambavyo ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru).
“Si siri mpaka hapa tulipofikia vyombo hivi vimefanya kazi kubwa, tunafanya uchunguzi tena kwa ajili ya kujiridhisha na kwenda ndani zaidi ili kujua undani wa suala hili, ili hata hatua zikichukuliwa dhidi ya mhusika ziwe za haki na si kuonea,” alisema.
Chanzo: Habarileo