Ripoti: Tanzania kinara wa utumwa Africa Mashariki

Ripoti mpya ya kimataifa kuhusu hali ya utumwa duniani imeitajaTanzania kuongoza Afrika Mashariki kwa kuwa na zaidi ya watu 350,000 wanaotumikishwa maeneo mbalimbali nchini.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, jana alikiri kuwapo kwa tatizo hilo akisema: “Ni kweli kuwa wafanyakazi wa ndani wanatumikishwa hapa nchini ikilinganishwa na nchi nyingine.”

Ripoti hiyo ijulikanayo kama ‘The Global Slavery Index 2014’, iliyotolewa nchini Australia Novemba mwaka huu, inaonyesha kuwa Tanzania inashika nafasi ya 14 barani Afrika na kuwa ya 33 duniani.

Imeitaja Uganda kuwa ndiyo inayoshika nafasi ya pili kwa kuwa na watumwa 135,000, ikifuatiwa na Rwanda (83,600), Burundi (72,300) huku Kenya ikiwa na watumwa 64,900.

Utafiti huo uliofanyika katika nchi 167 duniani, unatafsiri utumwa kuwa ni hali ya mtu kumhifadhi mtu mwingine na kumnyima uhuru binafsi kwa nia ya kumnyonya kwa njia ya madaraka, faida au kumsafirisha.

 “Mataifa mbalimbali yanatumia maneno tofauti kuuelezea utumwa mambo leo, ikiwa ni pamoja na kusafirisha binadamu, utumikishwaji, ndoa za lazima, kuuzwa kwa watoto. Maovu yote yanazungumzia jambo moja,” inasema ripoti hiyo.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa hivi sasa kuna watumwa milioni 35.8 duniani kote, kati yao milioni 14 wapo India, milioni 3 wapo China na milioni 2 wanapatikana Pakistan. Akizungumzia ripoti hiyo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba alisema hali imefika ilipo sasa kutokana na kukosekana kwa sheria kali na vyama vyenye nguvu vya kutetea haki za wafanyakazi hao.

Waziri Simba alisema kwa sasa ni jambo la kawaida kumsikia mtu akijisifu kuwa amekaa na mfanyakazi kwa miaka mitatu bila kwenda likizo.

“Mtu anasema ‘nimekaa naye miaka mitatu msichana huyu ni mzuri’ kwa hiyo nini? Anakaa kwako kwa sababu umeshindwa hela ya kumlipa akapange kama wafanyakazi wengine,” alisema.

Aliongeza: “Msichana anakuwa wa kwanza kuamka asubuhi na wa mwisho kulala usiku, akupikie mchana, usiku na akufungulie mlango unaporudi. Ndiyo maana wasichana wanawadhuru watoto wanaokaa nao.”

Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka na naibu wake, Dk Makongoro Mahanga hawakuweza kupatikana kuzungumzia ripoti hiyo baada ya simu zao kuita bila kupokelewa.

Kuhusu Afrika, ripoti inaonyesha kuwa Nigeria ndiyo inayoongoza kwa kuwa na watumwa 834,200, ikifuatiwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) (7,620, 900), Sudan (429, 000), Misri (393, 800) na Tanzania (350,000).
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad