UAMUZI juu ya maazimio ya Bunge kuhusu sakata la uchotaji fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow, utatolewa wiki ijayo na Rais Jakaya Kikwete.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Dar es Salaam jana, ilisema tayari Rais Kikwete amepokea Ripoti ya ukaguzi uliofanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ilisema Rais Kikwete pia amepokea nyaraka na ushauri uliotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano kuhusu sakata hilo.
“Rais Kikwete ameanza kupitia na kusoma nyaraka hizo, wiki ijayo atatoa maamuzi katika mambo yanayomhusu yeye na yale yanayoihusu Serikali, atayatolea maagizo na maelekezo ya namna ya kuyashughulikia.
“Baada ya kurudi nchini akitokea Marekani ambako alifanyiwa upasuaji wa tezi dume, Rais alianza kazi Desemba 8 mwaka huu,” ilifafanua taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, Rais Kikwete ameelekeza Ripoti ya CAG iwekwe hadharani ili umma uweze kuisoma na kujua nini kimesemwa, kupendekezwa na CAG.
Pia ameagiza ripoti hiyo itangazwe katika magazeti yanayosomwa na watu wengi na kwenye mitandao ya kijamii.
Akutana na viongozi wa dini