WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, wamesema baada ya hukumu ya Bunge sasa wanasubiri neno la Rais.
Viongozi hao waliyasema hayo jana, ikiwa ni siku chache tangu Bunge kupendekeza mamlaka za uteuzi ziwavue madaraka.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyowasilishwa bungeni na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ilionyesha viongozi hao walifanya makosa kadhaa na kusababisha uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Viongozi wengine ambao mamlaka zao za uteuzi zilitakiwa kuwavua nyadhifa zao ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye aliingiziwa Sh bilioni 1.6, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, Sh bilioni 1.6 na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja Sh milioni 40.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Profesa Muhongo alisema: “Sina maoni, sasa wewe unataka kujua nini… kwani wewe umeonaje na ni lazima nikujibu au unataka nikujibu porojo… sasa nakujibu kwamba kaulize Bunge kuhusu hilo suala la Escrow na kama una maswali kuhusu mambo ya umeme nenda Tanesco watakujibu.”