Harufu ya kuisha kwa mgogoro baina ya Zitto Kabwe na chama chake cha Chadema inanukia, lakini mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini anataka kuwapo na mazungumzo kubaini tatizo ili atakayebainika kuwa alifanya makosa awe tayari kuomba radhi hadharani.
Zitto alikiri bungeni kuwa amekuwa “akimiss” harakati zilizokuwa zikifanywa na vyama vya upinzani wakati wa Bunge Maalumu la Katiba, harakati zilizozaa Umoja wa Katiba ya Wananchi na kufurahia kuhudhuria kwa mara ya kwanza vikao vya umoja huo.
Zitto, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alipata fursa ya kuingia vikao vya Ukawa wakati wapinzani walipoungana tena kupambana dhidi ya wizi wa fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow, sakata ambalo liliwekwa bayana na kamati yake baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila kulifikisha bungeni, lakini hakudokeza lolote kuhusu Chadema.
Hata hivyo, mapema wiki hii, Zitto, ambaye Novemba mwaka jana alivuliwa nyadhifa zote kwenye chama hicho kwa tuhuma za kukihujumu, lakini akafanikiwa kulinda uanachama wake baada ya kufungua kesi mahakamani na kufanikiwa kupata amri ya kuzuia asijadiliwe.
Baada ya kuongoza PAC kuchunguza wa tuhuma za Escrow na kufanikiwa kulishawishi Bunge kufikia maazimio manane ya kuwashughulikia kisheria wahusika kwenye uchotwaji huo wa fedha, kumekuwapo na wito kutoka kwa baadhi ya wafuasi wa Chadema kutaka pande hizo mbili zimalizane.
“Kabla ya jambo lolote kufanyika, ili kukata kiu ya Watanzania wanaotaka kuona tunaondoa tofauti zetu, ni lazima kusema ukweli na kila upande kuwa tayari kuomba radhi hadharani pindi ikibainika ulifanya makosa,” alisema Zitto alipotakiwa kuzungumzia harakati hizo za kumrejesha Chadema.
“Ukweli wangu ndani ya Chadema ni nini? Lakini mimi ninaona sina kosa ndani ya Chadema. Ninachotaka mimi nielezwe ukweli bila chembe ya shaka makosa yangu mimi ni nini,” alisema na kuongeza:
“Nitakuwa tayari kuomba radhi hadharani kama ikibainika nilifanya makosa na kama ikibainika chama kilifanya makosa, nacho kiwe tayari kuomba radhi hadharani na ukweli uwe mbele katika maridhiano.
“Kama hakutakuwa na ukweli itakuwa vigumu kupata mwafaka. Mimi sina tatizo. Nirudie nilivyosema bungeni kuwa nina-miss sana (ninapenda sana kuwamo kwenye) harakati za mageuzi kipindi hiki za kuiondoa CCM madarakani.”
Hovyooo!
ReplyDelete