Afande Sele Unavyosema Daz Baba Atumii Madawa ya Kulevya Unazidi Kumpoteza

Mwanamuziki Daz Baba
Ingawa mimi ni shabiki wa kweli wa Afande, mtu ninayemkubali sana, huenda kwa sababu ya kuwa naye karibu kikazi, nimegundua tatizo lake moja la msingi, kuna wakati, kwa sababu anazozijua mwenyewe, huamua kuikwepa nafsi yake inayojulikana na kujivika asiyokuwa nayo.

Kwa hili, nimewahi kutofautiana naye mara kadhaa na ninachoshukuru, hakikuwahi kuharibu ukaribu wetu. Afande anasema asichotenda na anatenda asichosema! Wote tunajua, wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya wamejitumbukiza katika utumiaji wa madawa ya kulevya (Cocaine na Heroin) na wapo rafiki na ndugu zetu wamepoteza maisha kwa kuhusishwa na jambo hili, ingawa enzi za uhai wao, walikuwa wakikataa katakata kujihusisha nalo.

Nimewahi kusema mara kadhaa, watu hawawezi kumzushia mtu kitu kisichofanana na ukweli. Kwa mfano, tunao watu, ambao ni marafiki zetu, ndugu zetu na hata wafanyakazi wenzetu, wanatajwa kuwa ni mashoga, walevi, wezi na kadhalika. Hatuwezi kuamini moja kwa moja, lakini pia hatuwezi kupuuza. Kwa nini watajwe wao na siyo wengine?

Hatuna ushahidi, lakini utapuuza vipi unaposikia kila siku watu wanawataja Banzastone, Msafiri Diouf, Chid Benz, TID, Lord Eyez, Ray C na wengine kuwa wanakula ‘sembe’?Juzi, nimesoma mahali, mshkaji wangu Afande Sele akimtetea Daz Baba, yule mkali kutoka Kundi la Daz Nundaz, aliyetamba na vibao vingi vikiwemo Umbo Namba Nane, Elimu Dunia na kadhalika, kwamba kudhoofika kwake mwili hakutokani na utumiaji wa madawa ya kulevya, bali ni unywaji pombe uliopitiliza.

Ninamfahamu Daz Baba na ninajua Afande na Daz Nundaz ni washkaji. Anachofanya ni kujaribu kupooza sauti isiyokoma, inayopaza kuwa bwa’ mdogo anakula unga. Kama nilivyosema mwanzo, hatuna ushahidi, lakini kwa nini tupuuze sauti hii, inayotolewa na watu wanaomfahamu?

Kumsaidia Daz Baba na wengine wanaotajwa ni kuwaambia ukweli kuwa wanapoteza mwelekeo. Tuwaambie kuwa wanachokifanya sasa ni ujanja wa kizamani, ambao umewapoteza watoto wengi wa Kariakoo, Magomeni, Kinondoni, Mwananyamala, Ilala na Temeke, ambao leo hii wamekuwa ombaomba kwa watu ambao wakati wanaingia mjini kutafuta maisha, wao waliwaita wakuja!
Kwa hiyo ningetegemea Afande Sele, siku moja aachie kibao kinachowataja washkaji zake wabwia unga, akiwataka waache, kwa ajili ya Tanzania salama!
GPL

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad