Simba wakiwa na kikosi cha vijana ambacho kilikuwa chini ya Kocha Suleiman Matola huku wakiwa wanatazamwa na kocha wao mpya Goran Kopunovic aliyekuwa jukwaani akifuatilia mchezo huo, walishindwa kuelewana na kuwaruhusu Mtibwa kufunga bao kwenye dakika ya 41 ya mchezo mfungaji akiwa kiungo wao wa zamani, Henry Joseph.
Bao hilo lilifungwa baada ya kona ambayo iliunganishwa kwa kichwa na Ali Shomari kabla ya Henry Joseph kumalizia kwa shuti hafifu ambalo lilishindwa kuzuiwa na mabeki wa Simba na kipa wao Manyika Junior.
Mabadiliko yaliyofanyika kwenye kipindi cha pili ya kuwaingiza Danny Serunkumma na Jonas Mkude pamoja na Shaban Kisiga hayakutosha kuirudisha Simba mchezoni na hadi kipindi cha pili kinamalizika kuashiria mwisho wa mchezo huo Simba ilifungwa 1-0.
Michuano ya kombe la Mapinduzi inafanyika visiwani Zanzibar ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Mapinduzi ya visiwa vya Zanzibar na michezo yote imekuwa ikionyeshwa moja kwa moja na kituo cha Azam Tv.
~Millard Ayo