TAMKO LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAM TANZANIA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI KWA WATANZANIA WOTE, JUU YA MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA MBALIMBALI NA. 02, WA MWAKA 2014, HUSUSAN KUHUSU SEHEMU YA MAREKEBISHO KWENYE SHERIA YA TAMKO LA SHERIA ZA KIISLAM
Awali ya yote tunapenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Muumba wa Mbingu, Ardhi na vilivyomo, na Rehma na Amani zimfikie Kiongozi wa Ummah Mtume Muhammad (SAW).
Ndugu wanahabari,
Assalam Alaykum Warahamatul llah Wabarakatuh.
Tumekuiteni hapa kwa lengo la kueleza kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 02, wa mwaka 2014 haswa kuhusu marekebisho kwenye sheria ya tamko la Sheria za Kiislamu. Tunafahamu kuwa kuanzia tarehe 13 hadi 23 Mwezi huu wadau mbalimbali wataitwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba kwa ajili ya kuwasilisha mapendekezo yao, Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania tukiwa sehemu ya wadau muhimu tunapenda kuwaeleza kuwa mtiririko wa mchakato wa marekebisho ya sheria kwa mujibu wa muswada huu unaokusudia kutambua Mahakama za Kadhi Tanzania bara una kasoro kubwa na kwa dhati unaonesha wazi kuwa serikali haina nia ya kweli ya kuunda Mahakama ya Kadhi yenye hadhi kamili ya kimahakama na uthabiti wa kuwepo kwake na kuwa muswada huu ni hadaa nyingine ya serikali hii ya CCM kwa Waislamu kwa sababu zifuatazo:-
1. Malalamiko juu ya Mahitaji ya Mahakama ya Kadhi yana historia ya kupindishwapindishwa na serikali hii inayoundwa na CCM. Kwa mfano katika Ilani ya CCM mwaka 2005 iliahidi kuanzisha Mahakama ya Kadhi lakini kwa ghilba nyingi CCM haikutekeleza ahadi hiyo baada ya kuingia madarakani kwa hoja kuwa hili ni jambo la Kikatiba.
Hata hivyo mchakato wa Katiba mpya ulipokuja asilimia kubwa ya maoni ya Waislamu yalihitaji Mahakama ya Kadhi kuingizwa ndani ya Katiba, mapendekezo hayo yalikataliwa na Tume ya Jaji Warioba kwa hoja kuwa katiba inayotengenezwa ni ya Muungano na suala la Mahakama ya Kadhi si la Muungano hivyo lisubiri wakati wa kuandaa Katiba ya Tanganyika. Waislamu tukavumilia kuisubiri Katiba ya Tanganyika.
Lakini Bunge Maalum la Katiba likaikataa Katiba ya Warioba na kutunga Katiba Mpya Pendekezwa yenye mambo yote ya Muungano na yasiyo ya Muungano bila ya kuingiza Mahakama ya Kadhi kama ilivyoahidiwa na Tume ya Jaji Warioba. Bunge la Katiba lililokuwa linaundwa na wajumbe wengi wa CCM hawakuona umuhimu wa kutimiza ahadi yao ya kuweka Mahakama ya Kadhi katika katiba pendekezwa na kwa makusudi Mahakama ya Kadhi ikakataliwa na wajumbe wengi wa CCM walishangilia jambo hili ili hali wanajua dhahiri kuwa Waislamu hawakufurahishwa na uamuzi wao na pia kukiuka Ilani yao na ahadi kwa Waislamu.
Muswada huu ni sehemu nyingine ya hadaa kwa Waislamu kwani badala ya sheria kuanzisha Mahakama ya Kadhi kama ilivyo kawaida ya uanzishwaji wa mahakama zote duniani muswada huu umeliacha jukumu hilo kwa taasisi binafsi ili hali Mahakama ya Kadhi kama zilivyo mahakama zingine ni sehemu ya chombo cha dola katika mfumo wa Mahakama yaani “the Judiciary”, hili limefanywa makusudi kutokana na kutokuwepo na nia ya dhati ya Serikali ya CCM kuanzisha na kuona Tanzania Bara kunakuwa na Mahakama ya Kadhi madhubuti na ya ukweli.
2. MUSWADA umempa mamlaka “Mufti” kuteua makadhi na kutengeneza kanuni za Uendeshaji wa Mahakama ya Kadhi ili hali Mufti sio chombo cha kisheria.
Hakuna sheria inayounda ofisi ya Mufti isipokuwa uwepo wake unategemea katiba ya BAKWATA. Maana yake ni kwamba Mahakama ya Kadhi uwepo wake utategemea uwepo wa Katiba ya Bakwata inayounda ofisi ya Mufti. Kukiwa na mgogoro wa kikatiba Bakwata athari yake itaikumba na Mahakama ya Kadhi. Hakuna duniani mtu ambaye ofisi yake haiundwi na sheria kisha sheria ikampa mtu huyo madaraka ya kuunda chombo chenye mamlaka ya kisheria kama mahakama. Serikali ya CCM inalijua hili lakini imefanya makusudi kwa kusukumwa na nia yake ya kutopenda kuona Waislamu wanakuwa na Mahakama ya Kadhi ya ukweli iliyo madhubuti.
3. Kama tulivyoeleza hapo juu MUSWADA umempa Mufti mamlaka ya kutengeneza kanuni za uendeshaji wa Mahakama za Kadhi hili ni jambo la ajabu sana kwa ofisi ambayo haiundwi na sheria kuwa na mamlaka ya kutengeneza kanuni za kuendesha chombo cha kisheria ambacho ni Mahakama ya Kadhi. Hili ni jambo ambalo haliwezekani.
4. Kwa madaraka makubwa aliyopewa Mufti sheria haielezi ni nani mwenye mamlaka ya kumuondoa kadhi na wala haiweki sifa za kadhi na wala haiweki vigezo vinavyoweza kumuondoa kadhi yote hii inadhihirisha nia ya serikali ya CCM kuunda Mahakama ya Kadhi legelege na kiini macho.
5. MUSWADA unaeleza Waziri anayehusika na mambo ya sheria kupewa mamlaka ya kutunga taratibu za kutekeleza hukumu za Mahakama za Kadhi bila ya kushauriana na wanazuoni wa Kiislamu.
Japo katika sehemu ya maelezo ya muswada Mwanasheria wa Serikali ameeleza kuwa Waziri atashauriana na wanazuoni maelezo hayo ni hewa kwani si sehemu ya sheria.
6. MUSWADA umetoa hiyari kwa mtu kufungua shauri katika Mahakama ya Kadhi.
Jambo hili limekusudiwa kuifanya Mahakama ya Kadhi iwe butu na kutoa mwanya wa kutokea mgongano baina ya Mahakama ya Kadhi na mahakama za kawaida ikiwa kila upande katika mgogoro utaamua kufungua shauri katika mahakama tofauti. Hili lisingewezekana kama serikali ingekuwa na nia ya kweli ya kuunda Mahakama ya Kadhi madhubuti.
7. MUSWADA kuitaka Mahakama ya Kadhi ijiendeshe yenyewe:
MUSWAAD huu unaitaka Mahakama ya Kadhi ijiendeshe yenyewe badala ya kuendeshwa na serikali jambo ambalo halijawahi kutokea sehemu yeyote duniani chombo kama mahakama kujiendesha chenyewe.
Mahakama ya Kadhi itafanya jukumu la serikali katika kutafsiri sheria za Kiislamu ambazo ni sheria halali kutumika Tanzania hakuna mantiki yoyote kwa chombo hicho kujiendesha chenyewe kama ambavyo serikali ya CCM inataka kufanya.
Isitoshe uwepo wa hii Mahakama ya Kadhi kutaipunguzia serikali mzigo na msongamano wa kesi katika mahakama za kawaida jambo ambalo serikali inapaswa kugharamia uwendeshwaji wake. Serikali kukataa kuigharamia hii Mahakama ya Kadhi ilihali katika nchi hii upande wa Zanzibar serikali inaiendesha Mahakama ya Kadhi kunadhihirisha kuwa kuna nia ya kuidhoofisha mahakama hii ishindwe kujiendesha na kuwa na mahakama isiyokuwa na maana yoyote.
Zipo mahakama za makundi ya watu maalumu ambazo zinaendeshwa kwa pesa za serikali ambazo ni kodi za Watanzania wote. Mfano ni kama vile Mahakama ya Kazi, Ardhi, Biashara n.k. ni kwanini mahakama itakayotafsiri sheria za Kiislamu iwe nongwa?
8. UTAFITI unaonyesha kuwa suala la Mahakama ya Kadhi huletwa kila unapokaribia Uchaguzi Mkuu bila ya utekelezaji linazidi kutupa wasiwasi kwani inaonesha serikali ya CCM imeshazowea kuwacheza shere na kuwalaghai Waislamu na Watanzania kwa ujumla kwa maslahi yao ya kisiasa. Tabia hii ni hatari sana kwa mustakabali na ustawi wa taifa letu.
Hitimisho
Ndugu wanahabari, kwa maelezo yaliyobainishwa katika taarifa hii, tunahitimisha kwa kusema:
a) Jumuiya na Taasisi za Kiislamu (T) zimeukataa na kupinga mapendekezo ya marekebisho kwenye sheria ya tamko la Sheria ya Kiislam kama lilivyo katika MUSWADA wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali na. 02 wa mwaka 2014, mpaka utakapo andaliwa upya kwa kuhusishwa wanazuoni wa Kiislamu, wanasheria wa Kiislamu waliobobea na kwa kuzingatia maslahi ya Waislamu na taifa kwa ujumla na pia Mahakama ya Kadhi ni lazima iingizwe katika Katiba ili kuipa uthabiti.
b) Kwa kuwa katiba inayopendekezwa haitambui Mahakama ya Kadhi na inapinga sheria yoyote inayokwenda kinyume na katiba hiyo ikiwemo Sheria za Kiislamu kwa kauli moja na kwa nguvu kubwa Jumuia na Taasisi za Kiislamu (T) zitawahamasisha Waislamu na Watanzania kwa ujumla kuikataa kwa KUPIGA KURA YA HAPANA katiba inayopendekezwa muda utakapofika wa kuipigia kura.
Ndugu waandishi wa habari,
Ahsanteni sana kwa ushirikiano mliotupa.
Tunawatakia kazi njema katika ujenzi wa taifa letu.
Kaimu Katibu
………………………….
Jumuiya na Taasisi za Kiislam (T)