CCM yalaani vurugu kuapishwa kwa viongozi Serikali za mitaa

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimelaani vikali vurugu zilizofanywa na wafuasi wa Chadema na CUF kwa viongozi wa serikali za mitaa katika maeneo kadhaa nchini ikiwemo mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam na Mbeya.

Akizungumza na waandishi wa habari Katibu wa NEC; Itikadi na Uenezi CCM taifa, Nape Nnauye amesema vurugu hizo mbali na kuhatarisha na kuharibu mali pia zilizosababisha baadhi ya viongozi wa CCM kujeruhiwa vibaya na kupelekwa hospitali.

Amesema vurugu hizo zimetokea katika mkoa wa Mwanza ambapo Christopher Mgeta kutoka Mtaa wa Ibungilo na Pascal Charles wa Mtaa wa Kitangiri A katika wilaya ya Ilemela walivamiwa na kupigwa wakati wa kuapishwa.

Alieleza kuwa katika  Mkoa wa Dar es Salaam, Sultan Jeta wa mtaa wa Ukwamani katika jimbo la Kawe alifanyiwa fujo na wafuasi hao na Mtaa wa Msisiri A Kata ya Mwananyamala katika Jimbo la Kinondoni Juma Mbena alipigwa na kuvunjwa mkono.

“Katika Manispaa ya Ilala, wafuasi wa vyama vya upinzani walifanya vurugu wakati wa kuapishwa kwa viongozi wa serikali za Mitaa, jambo lililopelekea zoezi hilo kuahirishwa.

Nnauye amesema katika Mkoani Mbeya pia vurugu za aina hiyo zimetokea katika wilaya za Kyela na Rungwe ambapo wilayani Kyela zoezi la kuapisha viongozi wa serikali za mitaa lilishindika na kuahirishwa kutokana na vurugu za kurushiwa mawe zilizofanywa na wafuasi wa Chadema walioletwa kutoka katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo.

Aliongeza kuwa katika Kijiji cha Ilundo wilayani Rungwe wafuasi hao wa Chadema waliwapiga mawe viongozi na wanachama wa CCM na baadae kufyeka mashamba yao ya migomba na kusababisha vijana sita kujeruhiwa na kulazwa katika hospitali ya wilaya ya Rungwe kwa sababu ya hasira za kushindwa uchaguzi.

“Vurugu hizi ni mwendelezo wa tabia na mazoea ya vyama vya upinzani nchini kutoheshimu na kufuata sheria na taratibu za nchi,   tabia hizi si za kiungwana na ni uthibitisho wa kuharibikiwa na kufa kwa vyama vya upinzani nchini. Mara zote wamekuwa wakikataliwa na wananchi kwa kura, wao hukataa uamuzi huo wa wananchi kwa kufanya fujo na vitimbi, ”amesema Nnauye.

Wakati haya ya kijiri kesho Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), itakutana Jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kupanga ajenda zitakazojadiliwa kwenye mkutano wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama hicho  itakayokutana Zanzibar Januari 13.

Aidha msemaji wa jeshi la Polisi  SSP Advera J. Bulimba  amesema jeshi hilo halitawaonea huruma wale wote watakaohusika katika vurugu, kwani litawachukulia hatua kali za kisheria, badala yake limewaasa wananchi ambao hawakuridhika na uchaguzi huo kufuata taratibu husika.
Chanzo:Mwananchi

Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Hana lolote anajishaua tu anafikiri watu ni wendawazimu wafanye fujo tu bila sababu, waache kuchakachua matokeo

    ReplyDelete
  2. Nyinyi haohao mlishahujumu uchaguzi toka mwanzo sasa mlikuwa mnategemea nini? Kwa nini mnawaapisha walio shindwa ?.Na bado kiama chenu kinakuja.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad