Matokea ya Simba na Taifa Jang'ombe Kombe la Mapinduzi 2015 Zanzibar

WEKUNDU wa Msimbazi Simba wametinga kwa kishindo hatua ya nusu fainali ya kombe la Mapinduzi 2015 kufuatia ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Taifa ya Jang’ombe uwanja wa Amaan Zanzibar usiku huu.

Ibrahim Hajib amefunga mabao  matatu ‘hat-trick’ katika dakika ya 46, 62 na 75, wakati bao la nne limefungwa na Shaban Kisiga katika dakika ya 80.
Mapema kipindi cha kwanza Simba walianza kucheza mpira wa polepole wakigongeana pasi za uhakika na kufika eneo la hatari la wapinzani wao, lakini Maguli na Sserunukama walishindwa kujipanga vizuri na kupoteza nafasi nzuri za kufunga magoli.

Kiungo wa ulinzi, Jonas Mkude alipiga pasi rahisi na fupi fupi kwa viungo washambuliaji wa Simba  na mawinga wa pembeni na kuwafanya Simba wasogee zaidi eneo la hatari wapinzani.

Mabeki wa pembeni, Mohammed Hussein (kushoto) na Hassan Ramadhan Kessy (kulia) walipandisha timu na kupiga krosi, lakini bado washambuliaji wa kati hawakuwa na mipango mizuri.

Simba walitengeneza nafasi nyingi, lakini walikuwa na tatizo la umaliziaji.

Maguli alionekana kucheza chini ya kiwango, akishindwa kumiliki mpira vizuri na kupiga mashuti, lakini kocha Kopunovic aliendelea kumwacha mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika.

Hata hivyo, Simba walijitahidi kupiga mashuti yaliyolenga lango na mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika walikuwa wamepiga mashuti matano dhidi ya mawili ya wapinzani wao.

Katika kipindi hicho cha kwanza, Simba walimiliki mpira kwa asilimia 57 dhidi ya 43 za Taifa ya Jang’ombe.

Katika kipindi cha pili, Simba walianza kwa kushambulia lango la Taifa wakitafuta  bao la kuongoza.

Mapema dakika ya 46, Simba waliandika bao la kuongoza kupitia kwa Ibrahim Ajibu kufuatia kuukuta mpira eneo la hatari baada ya purukushani ya mabeki wa Taifa ya Jang’ombe na Danny Sserunkuma ambapo alipiga shuti lililozama nyavuni.

Purukushani hiyo ilitokana na pasi iliyopigwa na Kessy kwa Saimon Sserunkuma aliyempatia pasi ndugu yake Danny ambaye alipambana na mabeki wa Taifa na mpira kumkuta Ajibu akiwa eneo zuri.

Dakika ya 62 almanusura aandike bao la pili akijaribu kumalizia krosi ya Simon, lakini mlinda lango wa Taifa, Karim Musa aliokoa na kuwa kona.

Katika dakika hiyo hiyo, Ajibu aliandika bao la pili kwa shuti akimalizia mpira wa kona uliochongwa na Simon.

Dakika ya 73 Ajibu alimpiga chenga Hassan Soud eneo la hatari akielekea kufunga, lakini Abdallah Haji akamuangusha na mwamuzi akaamuru mkwaju wa penalty.

Akiwa tayari ana mabao mawili, Ajibu alikwenda kupiga mkwaju huo wa penalti katika Dakika ya 75 na kufanikiwa kufunga bao safi na kuandika ‘hat-trick’ ya pili katika mashindano hayo baada ya ile ya Saimon Msuva.

Msuva alifunga mabao matatu peke yake katika mechi ya ufunguzi ya kundi A Yanga ikishinda mabao 4-0 dhidi ya Taifa Jang’ombe.

Dakika ya 80, Shaban Kisiga aliifungia  Simba bao la nne kwa mpira wa adhabu ndogo baada ya Mohammed Hussein kufanyiwa madhambi.

Mechi nyingine tatu za robo fainali zitapigwa kesho uwanja wa Amaan Zanzibar.

Mechi ya mapema itaanza saa 9:00 alasiri ambapo KCC watachuana na Polisi Zanzibar.

Azam fc watashuka dimbani majira ya saa 11:00 jioni kucheza robo fainali ya tatu katika uwanja wa Amaan dhidi ya Mtibwa Sugar.

Mechi ya mwisho itapigwa majira ya 2:15 usiku ambapo Yanga wataoneshana kazi na JKU ya Zanzibar.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad