Wasanii waliofanikiwa kufanya vizuri miaka ya nyuma na hadi leo majina yao ni makubwa walikuwa na bahati sana. Pamoja na kwamba muziki wa zamani haukuwa wa kibiashara kivile, ulikuwa walau na usawa kwakuwa kama msanii alikuwa na ngoma nzuri basi wimbo wake ulikuwa ukichezwa bila hiyana.
Kukua kwa muziki na mabadiliko ya hapa na pale kumeufanya muziki uwe mgumu sana. Matatizo ni mengi na asilimia kubwa ya wasanii wanalalamika.
Tatizo kubwa ambalo makala hii itajaribu kulimulika ni kushamiri kwa rushwa na hongo au maarufu kama ‘hela ya promo’ ambayo watangazaji na madj wengi huhitaji ili kucheza ngoma za wasanii.
Kama imefika wakati hata msanii mkubwa kama Ben Pol analalamikia jambo hili, basi ujue kuwa limefika pabaya na wamiliki wa vyombo hivyo wanatakiwa kuwa wakali.
“Hongo inaua muziki, wanaposema huu muziki ni biashara wanatufumba, wanamaanisha kumwaga hela ndo kubaki kwenye kick zao,” alitweet Ben Pol. “Sasa hatushindani tena kutoa nyimbo kali bali tunashindana kumwaga hela…okay.. je, chipukizi masikini vipi, watatoka?” alihoji Ben Pol.
Ben Pol ni msanii mmoja tu kati ya wengi wanaokutana na vikwazo hivyo lakini kama kila msanii akiamua kuongea ya kwake, mambo mengi mazito yangeibuka. Na hebu fikiria tu kuwa kama Ben Pol ambaye kipaji chake kinajulikana na sikumbuki ni lini alitoa ngoma mbovu anaathirika na trend hiyo, vipi kwa wasanii wachanga?
Nafahamu kuwa wakati mwingine inakuwa sio rahisi kila wimbo kupata muda wa kutosha hewani, lakini kwa kupunguza playlist ya nyimbo za nje, kila ngoma kali ya msanii ina uhakika wa kuchezwa walau mara tatu kwa wiki.
Uongozi wa vituo hivi vya redio unatakiwa kuja na sheria zitakazowaongoza wafanyakazi wake kuhakikisha kuwa nyimbo zote zenye ubora na kali zinapata nafasi ya kuchezwa na kutoentertain kabisa ngoma mbovu.
Kama kila msanii mwenye kipaji na anayetoa ngoma kali atapata nafasi, hapo ndipo kiwanda chetu cha muziki kitakua.
~Bongo5