Ni ukweli kwamba bila jitihada sanaa haitakulipa. Msanii mwenye kuipenda kazi yake na mwenye dhamira ya kweli ya kuona matunda ya kazi yake, sharti ajitume sana ili afanikiwe. Nasisitiza; jitihada huzaa bahati.
Msanii anahitaji vitu vitatu aweze kufanikiwa. Kipaji kama silaha yake namba moja, juhudi kisha nidhamu. Ukiwa navyo hivyo, jihesabu kwamba umekamilika na ni suala la muda tu kufikia mafanikio yako unayoyaota.
Kipaji unacho, unajituma sana pia ni mwenye nidhamu, hapo utaonekana na kuoneshwa njia ya kupita. Hata hivyo, kwa Tanzania ni zaidi ya vitu hivyo vitatu. Kuna ufisadi mkubwa sana ambao umejikita katika sekta ya sanaa.
Ni mfumo; Watanzania hawana uchaguzi kwa kile wanachopenda, isipokuwa wanajikuta wanavutiwa na kile wanachokisikiliza na kukiona mara kwa mara.
Huu ni mfumo wa kifisadi; Unaua vipaji, unadidimiza aina ya sanaa, unakuza rushwa, hatimaye na sanaa yenyewe inauawa.
Radio, TV, magazeti lawamani; Waajiriwa ni vijana wadogo ambao hawana weledi mpana katika sanaa. Wengi wao wanajua Bongo Flava tu tena juujuu! Matarajio yetu hapo ni nini?
Kwa kawaida mtu hufanya kile anachokijua. Ni kwa sababu hiyo basi, waajiriwa wengi katika vyombo vya habari hujikita zaidi katika nyimbo na habari za Bongo Flava tu. Maeneo mengine ni maji ya shingo na utosi, watafanya nini?
Mbaya zaidi hawataki kujifunza, angalau waweze kujua aina nyingine ya sanaa, hivyo kuwa na uhodari wa kucheza nyimbo na kutoa habari kuhusiana na sanaa tofautitofauti. Wanaamini Bongo Flava ndiyo mpango mzima (ndiyo kila kitu).
NI MFUMO WA KIFISADI;
Bongo Flava ndiyo iliyoleta rushwa ya muziki kwenye vyombo vya habari. Baada ya kufanikisha mpango wa kuiaminisha jamii kuwa Bongo Flava ndiyo nambari moja sokoni, watangazaji, ma-DJ na hata waandishi nao wakaona fursa!
Wewe mwanamuziki kama hutoi chochote, hupati promo! Ni ukweli kwamba lazima mwanamuziki ajitangaze, kwa hiyo inamlazimu yeye au menejimenti yake ihonge ma-DJ, watangazaji na waandishi ili kupata promosheni.
Mfumo huo ukasababisha kupotea kwa vipaji vingi, ama kwa kuwa na mikono ya birika, au hawakuwa na uwezo wa kuhonga. Kwa kawaida, rushwa husababisha kizazi cha watu katili, kwamba bora ufe kama hutoi kitu kidogo.
Ni wimbo mzuri lakini kwa sababu hauna maslahi, acha tu upite, unatupwa kapuni! Ni mwanamuziki mzuri lakini kwa sababu hatoi hongo, ataishia kutajwa juujuu tu. Au wimbo wake utachezwa bila mwenye wimbo kutajwa.
Biashara ya muziki katika ulimwengu wa kileo, inategemea sana vyombo vya habari. Inapotokea vyombo vya habari havitoi sapoti kwa aina fulani ya muziki, jamii lazima ijielekeze kwenye ile aina ambayo inapewa nafasi kubwa kwa maana ndiyo inayosikika.
Mfumo huu wa kifisadi, ulianzishwa kisera, kwamba Hip Hop haiuziki, kwa hiyo watu wakaaminishwa hivyo, mwisho wakaamini. Likatoka tamko, muziki wa Dansi hauna vigezo vya soko la kisasa, haukubaliki sokoni. Kweli jamii ikaamini.
Hapa naomba nifafanue; Kuna mgonjwa mahututi aliyepata nafuu na kusimama tena baada ya kunywa kikombe cha Babu wa Loliondo. Mtu huyo alirudi nyumbani akiwa mzima, mwenye matumaini makubwa.
Aliondoka akiwa hajiwezi, amebebwa lakini alirejea akitembea. Wiki tatu baada ya kurudi nyumbani, alipoteza maisha kwa sababu aliacha dawa alizokuwa anatumia kwa imani kwamba amepona. Unadhani kwa nini aliamka? Ni imani baada ya kunywa Kikombe cha Babu!
Imani ndiyo kila kitu! Leo hii vyombo vya habari vikiamua kumpa promo ya nguvu Timbulo, inawezekana kabisa baada ya miezi miwili, akageuka bidhaa adimu na yenye thamani kubwa kuliko Diamond na Ali Kiba. Huo ndiyo ukweli.
Promo hujenga imani kwa hadhira! Kitu kinachotangazwa mara kwa mara tena kwa kushupaliwa, huvuta hisia za msikilizaji na mtazamaji kisha kujenga imani kwamba kitu hicho ni bora sana na bila kupanga hujikuta anavutiwa nacho.
Ukiamka Diamond, mchana Diamond, ukifungua gazeti Diamond, usiku Diamond, facebook Diamond, twitter Diamond, instagram Diamond, utajikuta unamfuatilia na kuvutiwa naye. Hapa ndiyo kumaanisha promo hujenga imani.
Yupo atakayesema simpendi, huyo ameshavutiwa na ujumbe umeshamfikia. Ni imani ndiyo inayofanya akina TID, Q Chillah, Banana Zorro na wengine wengi kuaminika ni zilipendwa, wakati uwezo wao ni hai, tena wenye kiwango cha juu kabisa. Tatizo promo!
Akitokea mwekezaji mwenye malengo ya kuvuna fedha kupitia kwa Banana Zorro, hivyo kuamua kumwaga noti kila kona, ujio mpya wa Banana utaimbwa kila kona. Atapambwa mpaka kwa sifa za kutisha. Ni promo, ni fedha, ni mwendo wa kisasa.
Ni mfumo huu wa kifisadi ulioibua rushwa ya ngono, mtoto wa kike hapewi nafasi ya kung’aa kimuziki kama ataendelea kuubania mwili wake. Yupo mtangazaji wa kike ambaye naye anaamua kujiweka kwa mwanamuziki anayempenda. Akiingia studio, full mashauzi ya kumsifia bwana’ke.
Wengne (watangazaji na ma-DJ) hawaombi rushwa ya moja kwa moja, ila wanaandaa maonesho kisha wanawaita wasanii ‘kupafomu’ bure, anayekataa, nyimbo zake zitapigwa fitna mpaka ziondolewe kwenye mzunguko wa kuchezwa.
JE, NI KWELI MUZIKI WA DANSI HAULIPI?
Nyakati ambazo akina Banza Stone, Ally Choky, Muumin Mwinjuma walifanya atakavyo kwenye soko la muziki Tanzania zimepitwa? Zama za FM Academia, Akudo Impact, Twanga Pepeta na kadhalika, zimekwenda wapi?
Si kweli kwamba muziki wa Dansi umeporomoka na kwama hauuziki. Ukweli ni kwamba vyombo vya habari viliamua kuugaya, au kwa lugha rahisi kuupotezea.
Mtanzania ambaye ni shabiki wa muziki, anataka asikie kwanza redioni kazi mpya za Twanga Pepeta, zimvutie ndipo akanunue CD na hata akisikia onesho Mango Garden, atapata mshawasha wa kwenda kuhudhuria.
Redioni Twanga hawasikiki, magazetin hawasomeki, runingani hawatazamwi, hiyo biashara watafanya na nani? Ukweli ni kwamba soko la muziki wa dansi linauawa na propaganda nyepesi ambayo ni kuacha tu kucheza nyimbo zao.
Ajabu ni kwamba mpaka makampuni ya kibiashara hasa yale yanayouza pombe, ambayo yalikuwa mstari wa mbele kudhamini bendi na maonesho ya muziki wa dansi, na yenyewe yameamini propaganda hiyo.
Kwa sasa, makampuni ya pombe yanajikita zaidi kwenye maonesho ya Bongo Flava kwa sababu ndiko wanakoaminishwa biashara ipo kubwa wakati si kweli.
Tafakari; Shabiki wa Bongo Flava yupoje? Ni kijana, ambaye akiwa kwenye onesho anaweza kusimama mwanzo mwisho. Kama siyo mwanafunzi ni kijana ambaye uwezo wake kununua pombe hauwezi kuwa wa kutisha. Akiwa na kampani, basi yupo na demu wake.
Shabiki wa dansi yupoje? Ni mtu mzima, akiwa kwenye ukumbi huwa na matumizi makubwa ya vilevi. Anaweza kuongozana na mkewe au wapambe ambao wote atawanywesha. Hii ndiyo sababu kwenye muziki wa dansi kukawepo mapedeshee! Wale watapanya pesa kama vile hazina kazi.
Kwa tathmini rahisi ni kwamba makampuni ya pombe pengine yangejikita kwenye muziki wa dansi, yanaweza kufanya biashara zaidi kuliko Bongo Flava kwa sababu ya kuangalia asili ya mashabiki na uwiano wa vipato pamoja na matumizi.
Hata hivyo, wameshaaminishwa kwamba Bongo Flava ndiyo mambo yote, unadhani watafanya nini? Hii ndiyo inaitwa promo katika mageuzi ya fikra.
Kampeni ilianza taratibu, kwamba nyimbo za Dansi ni ndefu, mwisho vile vipindi vyote vya Dansi viliondolewa. Vimebaki vituo vichache vinavyoendelea lakini kwa kusuasua.
UMEWASAHAU CHUCHU SOUND NA SAIDA KALORI?
Suala ni promo tu! Media ikiamua Mnanda ndiyo uwe muziki unaopendwa na kila Mtanzania itakuwa tu! Chuchu Sound wakati huo ikiundwa na Yusuf Chuchu (marehemu), Omary Mkali, Waziri Sonyo, Mao Santiago, Joniko Flower, Gabi Katanga (marehemu) na wengineo, ungeongea nini mbele yao.
Mduara uleule, wao waliuwekea vionjo na kuutangaza, baada ya hapo walitikisa kila kona ya Tanzania mpaka nchi jirani. Hapa ni kuthibitisha kuwa kila muziki unauzika na unalipa endapo utatangazwa kwa kiwango cha kutosha. Hakuna muziki usiolipa.
AT na miduara yake leo hii yupo wapi? Siyo kwamba harekodi kazi mpya, isipokuwa promo ni shida. Kijana huyu mwenye kipaji anakufa kimuziki hivihivi tunamuona.
Offside Trick walitajwa kama wapinzani wa AT, nao wamepotea. Mmoja wao akatangaza kuachana na muziki. Hayo ni matokeo ya kuzalisha wanamuziki wenye ‘stress’, wanafanya kazi nzuri lakini soko hakuna, jukwaa la kutangazia muziki wao limebanwa.
Je, Saida Kalori amesahaulika alivyojaza viwanja vya mipira kumuona akifanya vitu vyake? Kanda zake zikauzwa bei mbaya kuliko za mwanamuziki yeyote. Unadhani Saida hana uwezo tena? Ni promo tu! Jamii imeaminishwa amekwisha.
NANI KASEMA HIP HOP HAIUZI?
Baada ya kugusa maeneo tofautitofauti, sasa mjadala ukomee hapa. Nani mwanzilishi wa huu msemo kuwa Hip Hop haiuzi? Ni jamii hiihii ambayo inaaminishwa pia kuwa Reggae haina biashara.
Pengine hawajui au hawakuwepo kipindi marehemu Justin Kalikawe alipofanikiwa kuupenyeza muziki wake nchi nzima, japo hakukuwa na redio za kutosha. Alipofanya maonesho na watu walijaa, walimpenda na waliupenda muziki wa Reggae.
Unadhani kwa nguvu ya media iliyopo sasa, Kalikawe angekuwepo na kupata promo, Reggae ingekuwa wapi? Ukweli ni kwamba biashara bila matangazo ni ngumu. Akina Innocent Nganyagwa, Jhiko Man, wapo, hawana promo, kisha muziki wao unasemwa hauuzi.
Hip Hop ni muziki wenye nguvu, unauza na unalipa. Kitu cha muhimu ni kuangalia unaimba nini, yaani ule ujumbe wako unawezaje kuigusa jamii. Baada ya hapo, hakuna uchawi mwingine zaidi ya promosheni.
Hip Hop ni muziki wa harakati. Na kwa kawaida harakati ndizo huamsha na kukonga nyoyo za watu kisha kukusanya kundi kubwa. Unawezaje kusema Hip Hop haiuzi ikiwa ni muziki unaopendwa sana watu?
Hip Hop haiuzi kivipi ikiwa wasanii wa Hip Hop ndiyo huongoza kushangiliwa kwenye maonesho ya muziki? Ukitaka kuifanansha nguvu ya Ali Kiba na Diamond jukwaani, ukataka kuilinganisha na ya Weusi, MwanaFA, Roma, Prof. Jay jukwaani utakuwa unatania. Labda utakuwa hujui.
Kwa nini Weusi waonekane sokoni bei chee wakati jukwaani wanammeza Diamond? Hapa tatizo siyo nyota, ni promo tu! Weusi wakipewa promo ya kutosha, hawatakamatika.
JIBU UNALO;
Kama umesoma kwa makini, sasa unalo jibu ni kwa nini Niki Mbishi anatangaza kuacha muziki. Inahitaji mtu mwenye roho ngumu kuendelea kupambana na mfumo uliopo sasa. Wanamuziki wanafanya kazi, hazichezwi na bado wanaombwa pesa.
Inauma kuona mtu ambaye aliwekeza matarajio yake kwamba atafanikiwa kwenye muziki, anakumbana na kila aina ya changamoto, anamaliza miaka na bado changamoto haziishi.
Ukiwa unatabasamu, shangaa kwamba Miss Tanzania imefungiwa na Basata kwa miaka miwili, kwa kosa la udanganyifu wa Sitti Mtemvu, ila mpaka leo Prime Time Promotion wanadunda bila onyo wala adhabu wakati walimpandisha Davido kwenye jukwaa la Fiesta bila kibali.
By Luqman Maloto