Siri ya Wizi Mafuta ya Transfoma za Umeme yabainika, Kumbe Hayapikiwi Chips

Udaku Specially. 
Ile dhana ya kuwa mafuta ya kupoza transfoma yanaibwa na wauza chipsi, imebainika siyo ya kweli baada ya uchunguzi kuonyesha kuwa yanatumiwa viwandani kuendesha mitambo, kuchanganywa katika vipodozi na mengine yakisafirishwa nchi za nje.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa wanaoiba mafuta hayo ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pia huchukua nyaya za shaba katika transfoma hizo kwa ajili ya kutengeneza mapambo mbalimbali kama herini, mkufu na bangili.

Kutokana na wizi huo, mwaka jana pekee transfoma 34 zenye ukubwa mbalimbali ziliibiwa mafuta na shaba, hivyo kuisababishia Tanesco hasara ya Sh306 milioni.

Meneja Mwandamizi, Masoko na Mauzo wa Tanesco, Injinia Nicholaus Kamuleka alisema utafiti uliofanywa na wahandisi wa shirika hilo unaonyesha kuwa mafuta ya transfoma yanaibwa kwa ajili shughuli mbalimbali.

“Kazi ya mafuta ya transfoma ni kupoza nguvu ya umeme mkubwa,” alisema Injinia Kamuleka na kuongeza kuwa mafuta hayo pia huchanganywa na ya gari.

Transfoma kubwa moja inaweza kuwa na lita 200 za mafuta wakati dogo kabisa lina ujazo wa lita 40.

Kamuleka alisema pia hutumiwa na mafundi wa kienyeji kuchomelea vyuma ambao huyanunua kwa Sh5,000 kwa lita.

Mmiliki wa kiwanda cha chuma kilichopo Mikocheni ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema: “Sisi hatuwezi kuharibu transfoma na kuchukua mafuta, sisi tunaletewa hapa hapa.”

 Dhana ya chipsi

Injinia Kamuleka alikanusha kuwa mafuta ya transfoma hutumiwa na wafanyabiashara kukaanga chipsi na kusema kuwa harufu kali ya mafuta hayo isingefaa kwa matumizi ya kula.

Baadhi ya wafanyabiashara wa chipsi walisema ni vigumu kutumia mafuta hayo kwa kuwa yanauzwa bei ghali.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad