Waswahili wanasema ukweli unauma na wakati mwingine pamoja na msemwa ukweli kuwa kipenzi cha Mungu, huonekana mwenye dharau.
Hiki ndicho kilimkuta Diamond Platnumz kwenye ziara yake nchini Rwanda. Wakati akiongea na waandishi wa habari mjini Kigali, Diamond alidai kuwa wasanii wa Rwanda hawajitangazi kimataifa.
Kauli hiyo haikuwaingia vyema baadhi ya wasanii wa Rwanda akiwemo Jay Polly aliyekuwa mmoja wa wale waliomsindikiza kwenye show yake jijini humo.
Mshindi huyo wa msimu wa nne wa shindano la muziki la PGGSS, alidai ni ukosefu wa heshima msanii mgeni kudharau muziki wa Rwanda ambao alidai upo mahala pazuri.
“Kuna msanii mgeni atakayetumbuiza hapa leo. Nilisikia kwenye habari akidai kuwa wasanii wa Rwanda hawajui wanachokifanya,” alisema msanii huyo mbele ya maelfu ya wapenzi wa muziki mjini Kigali waliokuwa wamekusanyika kwenye uwanja wa Amahoro.
“Hilo lina ukweli gani ? Mnakubaliana naye? Inawezekanaje kuwa hatujui?” “Muziki wa Rwanda utaendelea kuwepo. Tutaupeleka kwenye hatua tunayotaka lakini kwa kuona tulipo sasa, hakuna mwenye haki ya kusema hatujui tunachokifanya,” aliongeza rapper huyo.
Hata hivyo gazeti la New Times la Rwanda limedai kuwa show aliyotumbuiza Diamond ilithibitisha wazi utofauti wake na wasanii wa Rwanda.
“Ni wazi kuwa show ya Diamond ilisimama ukilinginisha na zile za mwanzo,” mmoja wa mashabiki waliohudhuria show hiyo aitwaye Nina Uwase aliliambia gazeti hilo.
“Kiukweli, baadhi ya wasanii iliwabidi waumeze ukweli huo unaouma na kuungana na umati wa watu kumshangilia Diamond wakati alipokuwa akidondosha show ya nguvu ambayo huenda ilimfanya Jay Polly kufikiria mara mbili kauli yake aliyoitoa awali,” limeandika gazeti hilo.
~Credits:Bongo5