Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe amesema Watanzania wamepoteza imani na Jeshi la Polisi na ameliagiza kujitathmini na kutoa majibu kuhusu kukamatwa kwa vijana 1,200 wa kikundi cha uhalifu maarufu Panya Road.
Waziri Chikawe aliyekuwa akifungua mkutano mkuu wa mwaka kwa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi nchini, amelitaka jeshi hilo kujiuliza na kutoa majibu kutokana na madai kwamba baadhi ya vijana hao wamekamatwa kwa matakwa tu ya polisi.
Alisema kuwa anazo taarifa kuwa polisi wamejikita zaidi katika makusanyo, badala ya kuangalia usalama wa watu na ndiyo maana wamekuwa si watu wa kuzuia tena uhalifu kama inavyotakiwa lakini wanasubiri matukio yafanyike.
Alitaka polisi pia watoe sababu za kwa nini wananchi wanasema kuwa kumeibuka kitengo cha dhuluma, ambacho wamekibatiza kuwa ‘kuingia bure na kutoka kwa hela’, jambo linalotia doa chombo hicho.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Ernest Mangu, alisema jeshi hilo linakabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo uhaba wa vifaa na mafunzo katika kipindi hiki ambacho wizi wa mitandao unaonekana kupamba moto.
IGP Mangu alikiri kuwepo baadhi ya polisi ambao wanatumia vibaya viapo vyao na kusababisha shutuma kwa jeshi zima.
Hivi karibuni, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alitangaza kuwakamata zaidi ya vijana 1,500 kuwa madai ni Panya Road.