Vifurushi vipya vya mitandao: TCRA yatoa tamko na maagizo kwa makampuni ya simu

Mamlaka ya mawasiliano nchini, TCRA imetoa tamko kuhusiana na malalamiko kutoka kwa watumiaji wa huduma za simu nchini kufuatia kubadilika kwa vifurushi vya mawasiliano.

Malalamiko hayo yalikuja baada ya baadhi ya mitandao ya simu kupunguza ukubwa wa data anazopata mtumiaji wa simu anapojiunga na vifurushi vya muda wa maongezi, sms na data kwa pamoja.

Baadhi ya mitandao imekuwa ikitoa Mega Bytes 8 peke yake ambazo kwa matumizi ya kawaida ni ndogo mno.

“TCRA imechambua mpangilio wa vifurushi – tozo za zamani na mpya na kugundua kwamba ingawaje baadhi ya watoa huduma wamebadilisha bei, kwa ujumla bei za muda wa kuzungumza na idadi ya meseji hazikubadilika sana.

 "Hata hivyo, kuna upungufu mkubwa kwa idadi ya uniti za data (MBs),” amesema Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkoma kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Jumanne.

Kupitia kifungu cha 5 cha Kanuni za tozo (EPOCA Tariff Regulations) za mwaka 2011, TCRA imeyataka makampuni ya simu kuwasilisha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania gharama mpya wanazokusudia kutoza wateja wao kabla hazijaanza kutumika.

 Pia imeyataka kupitia upya bei na tozo mpya kwa kuzingatia mapendekezo hayo na kuwasilisha kwa Mamlaka kama inavyotakiwa kwa mujibu wa Kanuni za EPOCA za 2011 kuhusu tozo.

“TCRA inawaagiza watoa huduma kuhakikisha kwamba mabadiliko yoyote yanatekelezwa kidogo kidogo na sio ya ghafla ili kuepuka sintofahamu katika soko,” imesema.

“TCRA inawaagiza watoa huduma kuwapa wateja wao nafasi ya kuchagua mpangilio wa vifurushi tofauti kwa huduma wanazohitaji: Kifurushi cha mazungumzo, Meseji na Intaneti cha siku, siku saba au mwezi ambacho kinampa mtumiaji uhuru wa kuchagua kiasi ambacho wako tayari kulipia kwa mazungumzo, meseji na intaneti.”

“TCRA inawashauri watumiaji wa huduma za mawasiliano kuchagua vifurushi na mpangilio wa tozo ambao unafaa kwa matumizi yao.

"Watumiaji wanatakiwa kudai taarifa kamili kuhusu huduma wanazozilipia na waelewe taarifa za watoa huduma kuhusu bei na tozo, ikiwa ni pamoja na vigezo na masharti ya huduma.

"Mtumiaji asiporidhishwa na huduma anayopata anatakiwa alalamike – kwanza kwa mtoa huduma wake, na asiporidhika na ufumbuzi awasilishe malalamiko yake TCRA,” imesisitiza.

“Watumiaji wanashauriwa kuchukua fursa ya soko huria la mawasiliano nchini kama nafasi ya kulinganisha huduma na bei za watoa huduma na vifurushi wanavyouza kabla ya kuamua kujiunga na kifurushi chochote au huduma yoyote.

"Watumiaji wa simu janja zinazowezesha matumizi ya huduma nyingi, maarufu kama “smart phone”, kuwa makini wakati wa kuzitumia. Wahakikishe kwamba wanazima maeneo ambayo yanaweza kutumia data hata kama wakati huo hawatumii vifurushi vya data walivyonunua kwenye vifurushi.”

Katika hatua nyingine taarifa hiyo imetoa takwimu ya kuongezeka kwa matumizi ya simu na internet nchini katika kipindi cha miaka 10.

Imesema hadi sasa kuna laini za simu za mkononi zipatazo 31,862,656 ukilinganisha na laini 2,963,737 mwaka 2005.

“Idadi ya simu za mezani ni 151, ukilinganisha na 154, 420 mwaka 2005. Watumiaji wa intaneti wameongezake hadi kufikia 11,000,000 Desemba 2014 kutoka 3,563,732 mwaka 2008.
 
"Kwa sasa, kuna hamu kubwa ya matumizi ya intaneti na mwelekeo huu utaendelea; hasa kutakapokuwa na ongezeko la mitandao inayowezesha kutoa huduma za intaneti; na kuongezeka kwa mitandao ya jamii,” imesema.

“Wateja walionunua laini au ambao wanatumia huduma za simu kwa kuzungumza imeongezeka kwa asilimia 91 kutoka milioni tatu (3,000,000) mwaka 2005 hadi milioni 32 ( 32,000,000) mwaka 2014.

"Hii imewezesha huduma za simu kufikia asilimia 97 ya Watanzania ilipofika Desemba 2014; kutoka asimilia 10 mwaka 2005.
 
"Kwa upande mwingine, muda wa kuzungumza kwa simu, ukiwa umepimwa kwa dakika zinazotumika, umeongezeka sambamba na ongezeko la idadi ya watumiaji. Umefikia dakika bilioni 41 kutioka dakika milioni 506 mwaka 2005,” imeongeza mamlaka hiyo.

“Matumizi kwa upande wa meseji, yaani SMS na data pia yameongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka SMS zipatazo milioni 5 mwaka 2005 hadi SMS bilioni 10 mwaka 2014. Watumiaji wa intaneti wanaotumia simu za mkononi sasa wanafikia milioni 10.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad