SIKU moja baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kumuonya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, kwa tuhuma za kukiuka Katiba na kuanza kampeni za Urais kabla ya muda, kiongozi huyo ameibuka na kudai kuwa hana njia ya kuwazuia watu wasimuombe agombee Urais.
Pia Lowassa ametumia nafasi hiyo na kuwaomba wale wote ambao bado wana nia ya kumshawishi agombee nafasi hiyo ya urais, wasubiri kwanza hadi pale chama chake hicho kitakapotoa maelekezo.
Akizungumza na vijana 60 wa bodaboda kutoka wilaya ya Mbarali, Mbeya waliokwenda pia kumshawishi agombee nafasi hiyo, mjini Dodoma jana, alisema si vyema kwa maofisa wa chama kuzungumzia masuala ya wanachama wao kwenye vyombo vya habari wakati kuna vikao vya chama.
Alisema watu waliojitokeza na kumshawishi kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo ya Urais, hajawaita wala kuwalipa chochote kama inavyodaiwa na kwamba walikuwa wakifuata maneno ya Rais Jakaya Kikwete aliyoyatoa mkoani Ruvuma katika sherehe za maadhimisho ya miaka 38 ya Uhuru.
Alisema katika siku hiyo, Rais Kikwete aliwataka watanzania wawashawishi viongozi wanaoona wanafaa ili wajitokeze kugombea nafasi hiyo ya Urais.
“Mimi ni vigumu kuzuia mafuriko kwa mikono. Nazuia mafuriko kwa mikono, yanakuja mimi nayazuia kwa mikono, nitaweza kweli? Hawa watu sina hoja nao, sina cha kuwaambia,” alisema Lowasa.
Alisema tangu makundi hayo yaanze kujitokeza kumshawishi kuchukua fomu mambo mengi ya ajabu yamesemwa jambo ambalo linamsikitisha na kumshangaza kwa kuwa endapo kuna mtu wa chama mwenye hoja, ni vyema kuwasilisha kwenye vikao vya chama badala ya kuzungumza hadharani na kwenye vyombo vya habari.
Lowassa 'Mimi ni Vigumu Kuzuia Mafuriko kwa Mikono, Hawa Watu Sijawaita Mimi Wanakuja Wenyewe Kwa Kufuata Kauli ya Rais Kikwete'
0
March 26, 2015
Tags