KAIMU Kiongozi wa Shughuli za Serikali bungeni, Profesa Mark Mwandosya amewataka wabunge wasiligeuze Bunge kama eneo la maigizo, kutokana na kauli zao wanazozitoa wakati wanapotoa michango yao.
Alitoa kauli hiyo jana baada ya kuwepo majibizano makali ya wabunge wakati walipokuwa wanajadili azimio kuhusu kuridhia mkataba wa misingi na kanuni za utumishi wa umma na utawala barani Afrika, ambao uliwasilishwa bungeni na Waziri katika Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Celina Kombani.
Wanaomkebehi AG Profesa Mwandosya alikemea wabunge kutumia kauli zisizofaa na akatoa mfano baadhi ya wabunge kumshambulia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na kusema hatua hiyo haina tija kwa ustawi wa bunge hilo.
Mwanasiasa huyo aliwakumbusha wabunge kuwa AG ndiye mtu pekee, ambaye anaingia kwenye mihimili yote ya dola, ambayo ni serikali, Bunge na Mahakama, jambo ambalo aliwataka waone umuhimu wake.
“Kuna wabunge hapa walisimama wakamkemea mwanasheria mkuu wa serikali kwamba sio mwanasheria wao, hivyo asiwakosoe. Mimi nasema hapa tunakosea huyu ni mwanasheria wetu hapa bungeni,” alisema Profesa Mwandosya.
Alisema hata kama wabunge wana mwanasheria wao wa Bunge, haingii bungeni, hivyo ni lazima wasikilize ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wanapokuwa kwenye mijadala mbalimbali.
“Niseme kwamba hakuna aliye juu ya sheria, lakini chini ya sheria yupo mwanasheria mkuu wa serikali, ni vyema tumheshimu,” alisema Profesa Mwandosya.
Heshima bungeni Pia aliwataka wabunge kuvumiliana na kuacha kauli za ajabu bungeni, ambazo zinaweza kuwaaminisha wananchi kwamba Bunge ni uwanja wa maigizo.
“Hebu tusiwaaminishe wananchi kwamba bunge ni uwanja wa maigizo, hapa sisi ni waheshimiwa na tunatakiwa kuheshimiana na kuvumiliana,” alisema Profesa Mwandosya.
Awali, kabla ya kauli hiyo ya Profesa Mwandosya, Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) alimshambulia mbunge wa Lushoto, Dk Henry Shekifu kuwa hawezi kutoa hoja zenye mashiko bungeni kwa kuwa ana vyeti feki vya elimu.
Kauli hiyo ya Mkosamali ilitokana na Dk Shekifu kumwita mbunge huyo kuwa ni mtoto, hivyo anatakiwa awe na heshima kwa baadhi ya wabunge na kwa mambo ambayo yanafanywa na Serikali ya CCM.
Wajibizana bungeni Kutokana na kauli hiyo, Mkosamali alisimama na kuomba kumpa taarifa mbunge huyo “Mheshimiwa mwenyekiti naomba mbunge akome kuniita mtoto, mimi ni mbunge ambaye nimeshinda kwa kura nyingi na naongoza jimbo kama yeye.
“Mimi hapa ni mbunge na siyo mtoto, kwanza huyu mbunge hajui kitu maana hajawahi kukanusha kitabu na Msemakweli anayemtuhumu kuwa ana digrii feki na hivyo hawezi kuchangia jambo la msingi kwenye muswada huu,” alisema Mkosamali.
Kauli hiyo ya Mkosamali ilimfanya Dk Shekifu kusimama na kusema anamsamehe mbunge huyo, kwani kauli zake zinaonesha bado ni mtoto.
‘Msiligeuze Bunge uwanja wa maigizo kama wa Bongo Movies’ Mark Mwandosya
0
March 28, 2015