USHIRIKIANO: Kagame ammwagia sifa Kikwete

Kagame na Jakaya Kikwete
Rais wa Rwanda, Paul Kagame amemwagia sifa Rais Jakaya Kikwete kwa kuboresha huduma za Bandari ya Dar es Salaam na kuwezesha mizigo inayosafirishwa kwenda Rwanda kufika mapema zaidi kuliko ilivyokuwa miaka michache iliyopita.

Akizungumza kwa furaha wakati marais hao walipotembelea kitengo cha kushusha na kupakia mizigo cha TICTS bandarini hapo jana, Rais Kagame alisema hatua iliyopigwa ni mafanikio kwa Rwanda.

“Napenda nimpongeze Rais Kikwete kwa mafanikio yaliyopatikana bandarini, kazi ikiwa nzuri (bandarini Dar), huko kwetu Rwanda tunafaidika,” alisema Rais Kagame. Alisema Rwanda itaendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wananufaika kibiashara.

Rais Kikwete alisema tangu ameingia madarakani, ameitembelea Bandari ya Dar es Salaam mara nne, lakini ziara tatu za mwanzo hazikuwa za furaha kutokana na wizi, ucheleweshaji wa mizigo na malalamiko yaliyokuwa yamekithiri bandarini hapo.

Huku akionekana mwenye furaha, Rais Kikwete alisema Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inatakiwa ipongezwe kwa kufanikiwa kuwaondoa wezi waliokuwa wakiirudisha nyuma.

“Kwa hiyo kusikia habari nzuri zinazofanywa hapa mnanifurahisha sana. Kulikuwa na genge la wezi, sifa mbaya, meli zinakaa siku 23, mambo ya ajabu sana, leo meli zinakaa kwa muda mfupi na hakuna udokozi, kumbe mnaweza kuwa waaminifu,” alisema Rais Kikwete.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad