Wauza Madawa ya Kulevya Tanzania Kukiona cha Moto..Kunyongwa Ama Kupigwa Risasi Hadharani

Kijana Akitumia Madawa ya Kulevya
SERIKALI imewasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Udhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wa mwaka 2014, unaopendekeza wanaobainika kufanya biashara hiyo, watozwe faini ya Sh bilioni moja au kifungo cha maisha.

Hata hivyo, wabunge wameipinga adhabu huyo na kubainisha kuwa ni ndogo ukilinganisha na kosa la kukutwa na dawa hizo na kupendekeza adhabu iwe, kifo cha kunyongwa au kupigwa risasi hadharani.

Pamoja na hayo, wabunge hao, wameoneshwa kushangazwa na mamlaka za sasa kukamata watu na dawa za kulevya na kushindwa kuwachukulia hatua papo hapo, kwa madai ya kufanya uchunguzi wakati ushahidi kamili na vilelezo vipo.

Akiwasilisha muswada huo, bungeni Dodoma jana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama, alisema katika kuiongezea ukali sheria hiyo, adhabu za watu wote watakaokutwa, kutumia, kufadhili au kufanya biashara dawa za kulevya zimeongezwa na kuwa kali zaidi.

Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 12 cha Sheria iliyopo, adhabu ya kujihusisha na kilimo cha mimea ya dawa za kulevya (mfano bangi) ni faini ya Sh milioni moja au kifungo kisichozidi miaka 20 wakati Sheria inayopendekezwa imeweka adhabu ya faini isiyopungua Sh milioni 20 au kifungo kisichopungua miaka 30 au vyote kwa pamoja.

Alisema kwa kosa kubwa la kufadhili biashara haramu ya dawa za kulevya, sheria ya sasa inatoa adhabu ya faini ya Sh milioni 10 wakati Sheria inayopendekezwa imeweka adhabu ya Sh bilioni moja au kifungo kisichopungua miaka 30.

Aidha alisema kwa wale watakaokutwa na mitambo ya kutengenezea dawa hizo za kulevya Sheria imebainisha adhabu kuwa kifungo cha maisha na faini ya Sh milioni 200.

Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) wakati akichangia mjadala wa kupitishwa kwa Sheria hiyo, alisisitiza kuachana na adhabu ya faini badala yake, iwe kifungo cha maisha, kupigwa risasi hadharani pamoja na kunyongwa hadi kufa na kuachana na adhabu ya faini.

Alisema ana orodha ya majina na namba za nyumba wanakoishi wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini, lakini hawezi kuwataja bungeni hapo kutokana na hali ya sasa kuonesha kuwa mfumo mzima unawalinda wafanyabiashara hao.

Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), pamoja na kutaka watakaokutwa na dawa za kulevya kunyongwa au kupigwa risasi hadharani wiki mbili baada ya kuhukumiwa, pia aliitaka Serikali itafute mbinu ya kuondoa dhana kuwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo wanalindwa.

Aidha, Mbunge wa Chambani , Yusuph Salim Hussein (CUF) alihoji, “Lakini pia naomba niulize inakuaje mtu anakutwa amemeza kete tumboni za dawa za kulevya, anazitoa tumboni lakini hachukuliwi hatua eti kwa sababu ya uchunguzi, uchunguzi gani? Watu kama hawa wahukumiwe palepale...,”alisisitiza.

Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema) alisema ni wakati sasa Serikali kuanza kufanyia kazi hukumu za kunyongwa zinazotolewa na majaji kwa watuhumiwa wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi au kukutwa na kuuza dawa za kulevya ili kukomesha vitendo hivi.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Kama sheria hiyo itapitishwa bungeni katika muangalio wangu ni kuwa wahukumiwaji watakuwa ni samaki wadogo wadogo tu lakini samaki wakubwa hawatahukumiwa kwa hiyo enyi wabunge muifikiriye kwa kina sana hizo adhabu mnayoijadilia

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad