KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT – Wazalendo, Kabwe Zitto ameahidi chama chake kuendesha shughuli zake kwa uwazi, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku viongozi kufanya biashara na chama hicho, jambo ambalo limekuwa likidaiwa kufanyika ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambako aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu.
Ndani ya Chadema, mara kadhaa imekuwa ikidaiwa kwamba Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, amekuwa akifanya biashara na chama chake.
Akizungumza wakati wa hotuba yake ya uzinduzi wa ACT-Wazalendo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Zitto, bila kutaja chama wala jina la mwanasiasa yeyote, alisema chama chake kinapozungumzia wananchi kurejesha taifa mikononi mwao ieleweke kwamba wanazungumzia uwajibikaji.
“Chama cha ACT Wazalendo kimeelekeza kikanuni kwamba kila kiongozi wa chama lazima atangaze mali zake na madeni yake. Kila kiongozi lazima aweke wazi maslahi yake ya kibiashara na mengineyo wazi ili kila anapotenda au kusema jambo wananchi wajue maslahi aliyonayo au la katika suala husika.
“Viongozi wote wa kitaifa wa ACT Wazalendo wamefanya hivyo na tutaweka saini zetu mbele yenu kama mashahidi. Naomba Mwanasheria wetu aje hapa tutekeleze matakwa haya ya kikanuni.
“Fomu hizi zitakuwa kwenye tovuti ya chama ndani ya muda mfupi ujao ili kila mtanzaina aone. Kila Kiongozi wa Chama ambaye miiko ya uongozi inamtaja anapaswa kuwa amejaza fomu hizi na kuziwasilisha kwa Katibu wa Kamati ya Uadilifu katika ifikapo tarehe 30 Juni 2015.
“Tunapopinga viongozi wa umma kufanya biashara na serikali na hivyo kuwa na mgongano wa kimaslahi na kushamiri kwa ufisadi, hivyo hivyo tunapinga viongozi wa chama chetu kufanya biashara na chama. Ni marufuku serikali kugeuzwa kuwa genge la watu wachache wanaopora rasilimali za umma. Uadilifu tunaoutaka serikalini ni lazima uanzie kwetu tunaohubiri.
“Tutafanya haya kwa kubadilisha siasa zetu kuelekea kwenye masuala yanayowahusu wananchi; wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara ndogo ndogo, vijana, wanawake na wazee wetu.
“Tunataka kurejesha nchi yetu Tanzania kwa kujenga uchumi wa wote. Tunaporejea kwenye Azimio, hatusemi tunakwenda kutaifisha kila kitu na Serikali kuendesha shughuli zote za kiuchumi. Tunaheshimu na kuthamini sekta binafsi na mchango wake katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo.
“Tunamaanisha kuwa ni lazima Dola isimamie uchumi. Sio kazi ya Serikali kufanya biashara. Lakini tunamaanisha kuwa ni lazima kurekebisha baadhi ya makosa yaliyofanyika kwenye ubinafsishaji na hususan ubinafsishaji holela uliofanyika kwenye sekta ya Kilimo na kupora ardhi ya wananchi wetu na kuwageuza kuwa manamba kwenye ardhi yao wenyewe. Tunataka kutomokeza ukwepaji kodi,” alisema Zitto.
CHANZO: Raia Mwema
Zitto aichokoza Chadema na kuwapa somo wanachama wake
0
March 30, 2015