Wiki iliyopita, Meneja Uhusiano wa NHC, Yahya Charahani, akizungumza na Gazeti la Nipashe alisema kuwa walimpatia notisi Askofu Gwajima ya kuhama eneo hilo mwezi mmoja uliopita, muda ambao ulimalizika jana.
Jana mwandishi wetu alitembelea katika viwanja lililopo kanisa hilo saa 5:00 asubuhi na kukuta shughuli za kiibada zikiendelea kama kawaida.
Katika viwanja hivyo, kulikuwapo na mahema madogo madogo yaliyokuwa na waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Gwajima wakifundishana Neno la Mungu.
Kadhalika, mbele ya uwanja huo, kulikuwapo na jukwaa kubwa lililopambwa kwa vitambaa na hakukuwa na dalili zozote za kuhamisha vifaa vikiwamo vya muziki na spika kubwa.
Hata mwandishi alipoingia katika viwanja hivyo, alipokelewa na baadhi ya watumishi wa kanisa hilo na kuulizwa kama amekuja katika maombi au anahitaji huduma ya kiroho.
“Majeshi Majeshi, karibu tukuhudumie mpendwa, umekuja kwenye maombi au unahitaji huduma yoyote kutoka katika kanisa letu?,” mmoja wa wahudumu ambaye hakufahamika jina lake alimhoji.
Hata hivyo, Askofu Gwajima mwenyewe hakuwapo na hata alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi, iliita bila majibu na alipotumiwa ujumbe mfupi wa mkononi, pia hakujibu.
Kwa mujibu wa Charahani, NHC walimpatia notisi Askofu Gwajima ya mwezi mmoja kuondoka katika viwanja hivyo na kwamba notisi hiyo ilimalizika tangu Machi 9, mwaka huu.
Alisema baada ya kumalizika kwa notisi hiyo, NHC lilimpatia muda zaidi Askofu huyo ambao ulimalizika jana.
Hata hivyo, jana alipotafuwa Mkuu wa Kitengo cha Huduma na Mawasiliano wa NHC, Suzan Omary, kuelezea hatua gani zitafuata endapo Askofu Gwajima hatahamisha huduma za kanisa lake baada ya notisi kuisha, alieleza kuwa atafutwe leo kwa kuwa hakuwa ofisini wakati huo.
“Sipo ofisini leo (jana), nitafute kesho (leo), nitakupa ufafanuzi zaidi, na hata nikikuelekeza kwa mtu mwingine hatakusaidia kwa kuwa leo hakuna mtu ofisini,” alieleza Omary.
Toa Maoni Yako Hapa Chini
Inabidi lipelekwe buldoza la nguvu
ReplyDelete