MCHUNGAJI wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amewaacha waumini wake njia panda kufuatia kauli yake ya kuwataka wamsindikize Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati jijini Dar, jana alipokwenda kuhojiwa huku Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akiwa ametoa tamko la kuzuia waumini hao kukusanyika kituoni hapo.
Gwajima aliyetoa kauli hiyo kwa waumini wake katika ibada ya Jumapili iliyopita kanisani kwake, Kawe jijini Dar, alitarajiwa kufika kituoni hapo kujibu tuhuma za kumtusi Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinari Pengo.
Wakizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutoandikwa majina yao, juzi jijini Dar, baadhi ya waumini wa Gwajima walisema wanashindwa kufanya uamuzi wa kumsindikiza kiongozi huyo kwani jeshi la polisi limesema halitaruhusu mtu kumsindikiza.
“Kusema kweli tumebaki njia panda maana mchungaji amesema twende tumsindikize lakini Kova naye kasema jeshi la polisi litatumia nguvu kuwatawanya watu ambao watakaidi amri hiyo ya jeshi la polisi,” alisema muumini mmoja huku waumini wenzake wakiunga mkono.
Wakati Gwajima alipowataka waumini wake wamsindikize kituoni hapo, Kova alisisitiza kuwa kiongozi huyo wa dini anatakiwa kufika kituoni hapo akiwa na mwanasheria wake pamoja na watu wachache tu wa karibu hivyo kuwafanya waumini wengi wa kanisa la Gwajima kubaki njia panda.
Kupitia video inayomuonesha Gwajima akimtupia maneno makali Pengo, mchungaji huyo wa Ufufuo na Uzima alimtuhumu Pengo kuwa amewasaliti maaskofu wenzake waliotoa tamko la kuipigia kura ya ‘Hapana’ Katiba Inayopendekezwa kwa kile walichodai haikukidhi matakwa ya wananchi.
Askofu Gwajima Awaacha Waumini Wake Njia Panda...
0
April 10, 2015
Tags