Hatimaye Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewatoa hofu Watanzania kuhusu afya yake kwa kueleza kuwa anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa uchunguzi wa matatizo yake ya uti wa mgongo.
Kardinali Pengo pia amegusia nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa kuwataka watanzania kumchagua rais fukara kuliko anayetafuta nafasi hiyo kwa rushwa.
Alitoa kauli hiyo katika mahafali ya Saba ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam jana.
Alisema maradhi ya uti wa mgongo ambayo yamekuwa yakimsumbua kila yaligundulika Agosti mwaka 2013 baada ya kufanyiwa uchunguzi wa afya, Ujerumani.
“Hospitali ya Ujerumani ndiyo waligundua kuwa nyuzi mbili ndani ya uti wa mgongo zimechanika zinabana mashipa ya neva, kwa hiyo zikawa zinanisababishia maumivu ya mgongo.
“Kule Ujerumani walizirudisha katika nafasi yake lakini kwa bahati mbaya hawakufunga huku wakitegemea kuwa mambo yatakwenda vizuri kwa njia ya kawaida.
“Lakini kwa sababu ya kurukaruka nikajiona kama nimepona ila baada ya muda kidogo maumivu yasio ya kawaida yalirudi tena,” alisema kiongozi huyo wa kiroho.
Alisema maumivu yalipozidi Juni mwaka jana alisafiri kwenda Hospitali ya Manipal, Bangalore, India kwa uchunguzi zaidi.
“Walinihudumia vizuri na kwa sasa naendelea vizuri … kwa wale wanaojali uhai wangu nilipokwenda mara ya mwisho kwenye uchunguzi waliniambia kila kitu kimekaa kwenye nafasi yake.
“Madaktari walinielezea kuwa nisishangae maumivu ya mara kwa mara kwa sababu operesheni ilikuwa kubwa.
“Kwa sababu operesheni ya sasa itachukua muda kati ya miaka miwili hadi mitatu niweze kujisikia mzima kabisa. Kwa sasa naendelea vizuri sina tatizo zaidi,” alisema.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, Kardinali Pengo alisema ni kitu kibaya kama viongozi wanaowania nafasi ya urais wanatoa rushwa.
“Uongozi wa Taifa hauwezi kununuliwa kwa gharama yoyote… wanaoelekea kutoa rushwa baadaye watataka sisi wananchi tulipe zile gharama ambazo walikuwa wametugawia katika kutoa rushwa, afadhali waache kabisa.
“Ni vizuri tupate rais anayekuwa fukara lakini anayependa nchi yetu na hatatudai gharama ya kumchangua kama si hivyo gharama inaweza kuwa kubwa ikatusababishia matatizo,” alisema.
Kardinali Pengo pia alizungumzia matukio ya ugaidi na kuwataka wanaosambaza ujumbe fupi wa vitisho kuacha mara moja tabia hiyo kwa vile inawaweka wananchi katika hofu.
“Wanaweza kusababisha taharuki na mikanganyiko na kuleta madhara kwa wengi kwa kitu ambacho hakipo.
“Kama kuna hofu ya usalama sehemu yoyote inabidi tuwaachie wataalamu wa usalama waweze kuishughulikia kwa namna wajuavyo,” alisema.
Hata hivyo, aliitaka serikali kupitia Idara ya Usalama kuwa ya kwanza kuwahakikishia wananchi kuwa hakuna matukio hayo amani na utulivu viendelee kuwapo.
Pia aliwashauri wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Josesph kuwa wasisome kwa ajili ya kuajiriwa na serikali tu.
“Kuna nafasi za wataalamu wa sayasi na sanaa za kujiajiri katika chuo hiki … Chuo kikuu kizuri ni kile kinachoandaa wanafunzi kujiajiri,” alisema.
Mkuu wa Chuo hicho, Padre Aru Raji alisema chuo kinazidi kupanuka na mwaka huu kinatarajia kufungua Chuo Kikuu Sumbawanga na Chuo cha Afya na Tiba, Boko, Dar es Salaam.
Askofu Pengo: Nasumbuliwa na uti wa mgongo, Watanzania Chagueni Rais Masikini
1
April 24, 2015
Tags
… huyu kardinali vipi? mbona amebadili msimamo wake, hapa anawaelekeza waumini / watanzania wachague rais yupi. Kwa nini asiwaache WAFANYE MAAMUZI YAO WENYEWE JUU YA KUCHAGUA RAIS ALIYE MASKINI AU ALIYE TAJIRI kama ambavyo alitoa busara zake kinyume na maazimio ya maaskofu wenzake kwamba waumini / wananchi waachwe WAFANYE MAAMUZI YAO WENYEWE JUU YA KUPIGIA KATIBA PENDEKEZWA KURA YA NDIYO AU HAPANA. Nadhani kauli ya askofu Gwajima kuwa Pengo atakuwa anamkampenia mtu urais ina ukweli. Katika hao wanaotajwa au kujitaja kuwania urais yupi ni masikini? Jibu analo MUADHAMA, ASKOFU MKUU POLYCARP KARDINALI PENGO
ReplyDelete