Dereva wa bajaji, Alphonce Maurus, aliyebeba watu wanaodhaniwa kuwa watuhumiwa wa ugaidi, Kidatu wilayani Kilombero, ameweka hadharani namna alivyomfahamu mmoja wao.
Amesema mtuhumiwa ambaye aliuawa na wananchi baada ya kumjeruhi polisi, Hamad Makwendo, alijihusisha na mchezo wa kareti na masuala ya dini ya Kiislamu.
Dereva huyo huyo aliwaeleza waandishi wa habari waliofuatilia taarifa za kina za tukio hilo jana kwamba Makwendo alikuwa hana kazi maalumu ya kumwingizia kipato.
Maurus alitoa taarifa hizo katika kata ya Chikago, Kidatu wilayani Kilombero ambapo watu 11 walikamatwa na polisi msikitini wakiwa na silaha, milipuko na sare za jeshi.
Alisema siku ya tukio, saa tatu usiku, akiwa katika eneo lake la kufanyia kazi, walitokea watu 11 ambapo watano pamoja na mwenyeji ambaye ni marehemu, walipanda katika bajaji yake na wengine sita walipanda katika bajaji ya mwenzie.
Alisema watu hao walitaka kufikishwa katika msikiti wa Suni na kwamba wakati wote wa safari, mwenyeji wao ndiye alikuwa akizungumza lugha ya Kiswahili huku wenzake wakisikiliza bila kujibu kitu.
‘’Tuliwafikisha hadi eneo walilotaka na kisha tuligeuza na yule mwenyeji wao, ambapo tulipofika manyasini tulisimamishwa na polisi wakitaka kujua tumetoka wapi na tunakwenda wapi.
“Yule mwenyeji alishuka na kuanza kukimbia jambo lililofanya askari kuanza kumkimbiza huku na sisi tukifuatilia nyuma,’’ alisema.
Alisema Makwendo alipofika mbele alimkata polisi mmoja na jambia na ndipo polisi walifanikiwa kumpiga risasi na wakamchukua na walimchukua na kumpandisha katika gari lao.
Maurus alisema wananchi walifika katika eneo hilo na kuzingira gari hilo na kumshusha mtu huyo huku wakitishia kuchoma moto gari la polisi.
Akizungumzia mwonekano wa watu hao, dereva huyo alisema walivalia mavazi ya jamii ya Kihindi, maarufu kama Punjabi, huku umri wao ukionekana kati ya miaka 20 na 25 tofauti na mwenyeji wao alieyonekana na umri wa takribani zaidi ya miaka 30.
Kwa upande wake, askari aliyejeruhiwa, Koplo Nasoro Dabi, ambaye amelazwa katika zahanati ya Polisi Mkoa wa Morogoro, alisema siku ya tukio, akiwa na askari wenzake walisimamisha bajaji aliyopanda Makwendo.
Alisema baada ya bajaji hiyo kusimama, mtuhumiwa huyo alikimbia, hali iliyoashiria kuwa ni mhalifu hivyo kuwalazimu askari watatu, akiwemo yeye kumfukuza.
‘’Wakati tukimkimbiza, nilikuwa mbele na kwamba tulipofika katika giza alichomoa jambia na kunishambulia. Askari wenzangu waliokuwa nyuma yangu walifyatua risasi na zingine kupiga juu hali iliyosababisha wananchi wengi kujitokeza kumpiga na kumchoma moto,’’ alisema.
Alisema wakati tukio hilo likiendelea askari wengine walifanya mawasiliano na Mkuu wa Kituo cha Ruhembe kwa ajili ya kuwaongezea nguvu.
Naye Mganga Mkuu Zahanati ya Polisi Morogoro, Mrakibu Thomas Kawala, alisema walimpokea askari huyo anaendelea na matibabu.
Kawala alisema askari huyo alifika zahanati hapo akiwa na maumivu makali lakini kwa sasa anaendelea vyema na matibabu.
Mmoja wa Kiongozi wa Msikiti wa Masjid Salah Al – Fajih , Mohamed Manze, alisema wakiwa viongozi na waumini, hawakuwa na taarifa zozote za ujio wa watuhumiwa hao na kwamba katika msikiti huo wako vijana wanne ambao huwa wanalala na kujisomea hapo.
Alisema siku ya tukio watuhumiwa hao walifika msikitini hapo saa nne ambapo ibada ya mwisho ilikwishafanyika na waumini kutawanyika, ambapo walikuwa wamebakia vijana hao peke yao.
Manze alisema walitumia mwanya huo kuingia na kujihifadhi bila taarifa zozote kwa uongozi wa msikiti, jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu za msikiti huo.
Hata hivyo, alisema wakiwa waumini wa msikiti huo, hawakupendezwa na suala hilo kwa kuwa limewachafua na kuwaharibia sifa na kwamba Makwendo hakuwa muumini wao.
Alisema hawana nasaba na kikundi chochote kinachojihusisha na uhalifu na kwamba wanalaani vibaya watu wanaotumia dini katika masuala hayo ya uhalifu.
Dereva Wa Bajaji Asimulia Jinsi Magaidi 10 Walivyonaswa Morogoro Wakiwa Na Silaha Msikitini............Imamu Awakana 'Magaidi' Hao
0
April 17, 2015
Tags