Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ambaye jina lake linatajwa kutaka kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, anaelezwa kutamani kuingia katika hatua za mwisho za kinyang’anyiro hicho na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Vyanzo vya habari ndani CCM vinasema kwamba Membe amekua akionyesha kutamani kuingia katika hatua ya 'tatu bora' pamoja na Lowassa ili aonyeshe uwezo wake ndani ya chama hicho, tofauti na wapinzani wake wanaodai hana nguvu kisiasa na hawezi kushindana na Lowassa ndani ya chama.
"Membe anatamani sana kama akigombea aingie na Lowassa katika hatua ya mwisho maana anatamani aonyeshe uwezo wake, kama alivyowaonyesha katika uchaguzi wa kuingia NEC (Halmashauri Kuu ya CCM) mwaka 2012, ambao walimpiga vita na kutumia fedha nyingi lakini akapata kura za kutosha bila kampeni ya nguvu na kuwatia aibu," anasema mtoa habari huyo ndani ya CCM.
Katika uchaguzi huo wa mwaka 2012 ambao Lowassa hakugombea katika ngazi ya Taifa na badala yake aligombea kupitia Wilaya ya Monduli, Membe alipata kura 1,455 ikiwa ni asilimia 74 ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM pamoja na kupigwa vita na wanasiasa ili asipite na kuingia NEC.
Mbio za Urais CCM: Benard Membe Ataka Jina la Edward Lowassa Lisikatwe.......Atamani Akutane Naye Tatu Bora Ili Amwonyeshe Uwezo Wake
0
April 12, 2015
Tags