Mgomo wa Madereva umeanza rasmi leo katika maeneo mbalimbali nchini kama ambavyo muungano wa madereva wa vyombo vya usafiri waliahidi wakidai kutotatuliwa kero zao na serikali.
Sababu kubwa ya madereva hao kugoma ni kuishinikiza serikali kuweka mfumo mzuri wa ajira na kupinga kanuni inayowataka kurudia kusoma katika chuo cha taifa cha usafirishaji,NIT kila leseni zao zinapokwisha muda.
Madereva hao wanadai malalamiko yao makubwa ni kitendo cha Serikali kuongeza kifungu kidogo katika sheria mpya ya mwaka 2015 namba 31 inayowataka madereva wote wenye leseni za madaraja E,C1,C2,C3 na C kurudi darasani kila baada ya miaka mitatu kuongeza utaalamu katika fani hiyo ya udereva ili kupunguza ajali za mara kwa mara zinazotokea.
Umati wa abiria wakiwa kwenye kituo cha daladala cha Darajani-Ubungu huku kukiwa hakuna daladala yoyote inayofanya kazi baada ya kutokea kwa mgomo wa madereva wa Daladala jijini Dar.
Baadhi ya abiria wakiwa wamepanda magari ya mizigo baada ya kukosekana kwa daladala maeneo yote ya jiji la Dar es Salaam leo asubuhi.
Mmoja wa abiria akiongea na dereva wa kibasi kidogo kuangalia kama kuna uwezekano wa kupata usafiri maeneo ya Mwenge jijini Dar.