Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limetangaza mgawo wa umeme kwa siku tisa katika baadhi ya maeneo kutokana na upungufu wa nishati hiyo katika Gridi ya Taifa.
Hali hiyo imetokana na maombi ya Kampuni ya Pan African Energy (PAT) inayosimamia uzalishaji wa gesi asilia Songosongo kusimamisha uzalishaji kwa nyakati tofauti ili kufanya matengenezo na kubadilisha baadhi ya vifaa kwenye mitambo yake.
Taarifa ya shirika hilo kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana ilisema shughuli hiyo itafanyika kwa siku tofauti kati ya Aprili 6 na Mei 10.
“Hivyo Shirika linawatangazia wateja wake waliounganishwa kwenye mfumo wa gridi ya Taifa kwamba kutakuwa na upungufu wa umeme kwa baadhi ya maeneo kutokana na matengenezo hayo yanayofanyika kila mwaka,” ilisema.
Tanesco inategemea gesi hiyo kuendesha mitambo yake ya Ubungo 1, Ubungo 2 na Tegeta yenye uwezo wa kufua megawati 245 na kuendesha mitambo mingine ya umeme ya Songas yenye uwezo wa megawati 180.
Taarifa hiyo ilisema pamoja na kutumia vyanzo vingine vya kufua umeme kama maji na mafuta, katika kukabiliana na matengenezo hayo, ukosefu huo wa gesi utaathiri ufuaji wa umeme kwa siku tisa. Hata hivyo, taarifa hiyo ilisema upungufu huo kwa kila siku utagawanywa kidogokidogo kwenye mikoa iliyopo kwenye gridi na hautaathiri upatikanaji wa umeme kwa mkoa mzima.
Akizungumzia mgawo huo, Meneja wa Mawasiliano Tanesco, Adrian Severin alisema ukiondoa tatizo hilo la ukarabati wa miundombinu ya gesi, shirika lake halina tatizo la kuilazimisha nchi kuingia katika mgawo kwa sasa.
Pia, aliitaja mikoa ambayo haitaathiriwa na mgawo huo kuwa ni Kagera, Ruvuma, Kigoma, Lindi, Mtwara na Wilaya ya Loliondo, Arusha.
CHANZO: Mwananchi
TANESCO Yatangaza Mgawo wa Umeme wa Siku Tisa Kutokana na Upungufu wa Nishati hiyo Katika Gridi ya Taifa
0
April 10, 2015
Tags