Kusambaa kwa taarifa za uwezekano wa kutokea kwa shambulio la kigaidi katika miji ya Tanzania, ikiwemo Dar es Salaam na Mwanza, kumesababisha baadhi ya taasisi muhimu kama vyuo vikuu na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuchukua hatua za kujihami.
Taarifa zilizotufikia jana zilieleza kuwa Tanesco na baadhi ya vyuo, vimeweka taarifa ya tahadhari na kutoa masharti kwa wafanyakazi na wanafunzi, ya namna ya kujilinda.
Mtandao huu ulimuuliza Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba, kuhusu hatua hizo ambapo alikiri shirika hilo kuchukua hatua za ziada kujihami na uwezekano wa shambulio hilo.
Mramba alisema wamechukua hatua hizo za kiusalama baada ya kuwepo kwa tetesi za uvamizi hasa baada ya kuwepo kwa tukio la nchi jirani ya Kenya, ambako wanafunzi 148 waliuawa.
“Kutokana na tishio hilo, tumeona ni vyema tuchukue hatua mapema… si lazima yatokee ndiyo tuchukue hatua, tumeona ni vyema kujihami kwa kuimarisha ulinzi katika vituo vyetu.
“Kuna baadhi ya maeneo yetu ni maalumu na yakiwa na athari za kiusalama ni hatari kwa nchi nzima... hivyo ni vyema tuchukue tahadhari kubwa maana kunapotokea tatizo, huathiri nchi nzima,” alisema.
Vitambulisho
Alisema wamewaelekeza na kuwasisitiza watumishi wao kuimarisha ulinzi wao na katika maeneo ya kazi. “Kwa kawaida tuna vitambulisho vya ofisi lakini kuna watu wengine walikuwa hawavai, ila kwa sasa tumesema ni lazima kila mfanyakazi avae kitambulisho wakati wote,” alisema.
Katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IMF) hali ya ulinzi ilikuwa imeboreshwa, ambapo kila mwanafunzi alitakiwa kuvaa kitambulisho chake awapo katika maeneo ya chuo, ili mgeni yeyote atambulike kwa haraka.
Uongozi wa chuo hicho ulichukua tahadhari kwa kuweka tangazo kumtaka kila mwanafunzi achukue tahadhari pale anapoona mtu ambaye ana shaka naye au kitu cha kutia shaka; pia taarifa hiyo iliwataka wanafunzi kuvaa vitambulisho vyao.
Ukaguzi
Mramba alisema mgeni yeyote atakayefika katika ofisi za shirika hilo kwa sasa ni lazima akaguliwe na ajulikane anatoka wapi na anaingia ofisini kwa sababu gani. Mbali na ofisini, alisema ukaguzi pia utafanyika kwa watu wote wanaoingia kwenye mitambo.
“Tumeimarisha askari wetu ili kuhakikisha rasilimali za Tanesco ambazo ni za nchi zipo salama.”
Katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), katika lango kuu la kuingilia ofisi mbalimbali za utawala, kumewekwa ulinzi na watu wote wanaoingia na kutoka, wamekuwa wakikaguliwa kwa vifaa maalumu tofauti na huko nyuma.
Matangazo ya tahadhari
Aidha UDSM, kama ilivyo IFM pia kumebandikwa tangazo lililotolewa na Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho (Utawala), Profesa Cuthbert Kimambo, likieleza kuwa hatua madhubuti zinachukuliwa na zitaendelea kuchukuliwa katika kuimarisha ulinzi.
Alisema kutokana na taarifa za tahadhari kuhusu matukio ya uhalifu yenye taswira ya kigaidi katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu, ni jukumu la kila mwana jumuiya ya chuo hicho kuwa macho kusaidia kuimarisha ulinzi na usalama.
“Baadhi ya hatua zinaweza kuleta usumbufu kwa wengi wetu. Taarifa zitatolewa inapowezekana, lakini tunaomba uvumilivu na ushirikiano wenu ili kuhakikisha usalama wetu,” ilisema taarifa hiyo ya Profesa Kimambo.