Ukawa wavuruga Bunge Dodoma, Wadai Hawataki Kuburuzwa Buruzwa na Kupelekeshwa
0
April 02, 2015
Wabunge wa upinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) jana walianzisha tafrani bungeni na kusababisha kikao cha Bunge kuvunjika saa 5.18 asubuhi baada ya kusimama na kupaza sauti wakishinikiza Serikali itoe kauli juu ya hatima ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura na upigaji wa Kura ya Maoni kupitisha Katiba Inayopendekezwa.
Huku wakiwa wamesimama walikuwa wanapiga kelele wakisema, ‘hatutaki kuburuzwa’, ‘tumechoka kupelekeshwa’, Watanzania wapo njia panda’ na ‘tunataka majibu,’ ‘Bunge lisitumiwe kuilinda Serikali’, ‘Waziri Mkuu yupo bungeni kwa nini asitoe kauli’ na maneno mengine mengi bila mpangilio.
Wabunge hao wa vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na CUF, kwa umoja wao walimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutoa majibu hayo muda huohuo, kabla ya jioni kutoa hutuba na kuahirisha mkutano huo wa 19 wa Bunge.
Baadaye jana usiku katika hotuba yake ya kuahirisha Bunge hadi Mei 12, utakapoanza Mkutano wa 20, Waziri Mkuu Pinda alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itatoa taarifa siku za hivi karibuni kuhusu upigaji wa kura ya maoni.
“Ni dhahiri muda uliobaki kuanzia sasa ni mfupi lakini Tume ndiyo itakayotujulisha ratiba kamili,” alisema.
Tags