Urais 2015: CCM Imejiandaa na Changamoto za Kumkubali au Kumkataa Edward Lowassa?

Ni ukweli usio na shaka kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu wa zamani, Ndugu Edward Ngoyai Lowassa ana dhamira ya kugombea kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chake cha CCM.

 Ni ukweli usio na shaka pia kwamba ili afikie hatua ya kuwa mgombea urais wa CCM ni lazima kwanza ashinde kwa kuruka na kuvuka “viunzi” na “vigingi” vya Kamati ya Maadili, Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu, ambavyo vyote hivyo ni vyombo vya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kwa mujibu wa hali ya hewa ya kisiasa katika nchi yetu kwa sasa, inaonekana wenye “nia” ya kuiomba CCM ikubali kuwakilishwa na wao kwa nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika, inshaa-Allah, mwishoni mwa mwaka huu, wako wengi pengine wakaizidi idadi ya “wasaka urais” wa CCM waliojitokeza mwaka 1995 na 2005.

Hapo tunaona kwamba “ushindani” ndani ya CCM juu ya ni nani haswa aiwakilishe, utakuwa mkali na mgumu mno.

Swali ambalo ni muhimu na lazima litafutiwe majibu mapema ni kumtafakari kila mgombea atakayeomba “ridhaa” ya CCM kuiwakilisha ni ipi faida ya kuiwakilisha CCM na yapi madhara ya kutokuiwakilisha; hiyo ni tafakuri ambayo ni muhimu kila mmoja wao kufanyiwa.

Kalamu yangu kwa leo imeona iikumbushe CCM kufanya tafakuri hiyo kwa Mheshimiwa Edward Lowassa kabla ya hao watarajiwa wengine. Ninapendekeza tafakuri hiyo ianze kwa Mheshimiwa Lowassa kwa sababu:

(a) Ndiye mgombea mtarajiwa pekee ambaye anaonekana kuwa na wapenzi na mashabiki wengi mpaka hivi sasa.

(b) Ndiye mgombea mtarajiwa pekee ambaye tayari ameshatamka kwamba katika uongozi wake ataanzia pale ambapo Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete atakapoishia (hiyo ni dalili kwamba “piga ua” atagombea tu).

(c) Ndiye mgombea mtarajiwa pekee ambaye tayari amefuatwa na kushawishiwa na makundi kadhaa wa kadhaa.

(d) Ndiye mgombea mtarajiwa pekee ambaye wasifu wake na historia yake inamtofautisha na wagombea watarajiwa wengine.

Si sahihi hata kidogo kumdharau au kuidharau jamii hiyo ya kitanzania iliyojenga imani kwake, na ndipo nikaonelea nianze “uchokozi” mapema kwa njia ya swali kwamba: Je, CCM imejiandaa na changamoto za kumkataa au kumkubali Lowassa?

Katika hali ya kawaida na kwa kutumia akili tu ya kuzaliwa, endapo Chama cha Mapinduzi (CCM) kitamptisha Mheshimiwa Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao, itapambana na changamoto kadhaa.

Lakini hata kama CCM watakataa kuwakilishwa na Mheshimiwa Lowassa, bado pia zitakuwepo changamoto kadhaa. Kwa muktadha huo, kumkubali Mheshimiwa Lowassa ni tatizo, na hata kumkataa ni tatizo pia.

Mfano wa Mheshimiwa Lowassa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ni kama “tonge tamu” la chakula cha moto ambalo ukilimeza utaungua na kulitema huwezi kwa sababu ni tamu na unalihitaji.

Kazi kubwa sana ambayo watapambana nayo viongozi wa CCM ni kuyapima madhara na faida kwa kutumia kipimo huru kisichohusishwa na “shinikizo” lolote lile.

Pamoja na kwamba CCM ndio wanaowajibika na kazi ya kuufanya utafiti huo, lakini kutokana na mazingira ya siasa za kitanzania kwa sasa tunaweza kuyapima yale ya “juu juu” ambayo muonekano wake uko wazi. Halafu yale ambayo ni ya “ndani zaidi’ yatatamkwa na wenyewe (makada na makomredi wa CCM).

CCM ikithubutu kufanya “mizengwe” na hila yoyote kumkataa Mheshimiwa Lowassa kiasi kwamba, yeye Lowassa na wafuasi wake wakajiaminisha kwamba “wameonewa”, basi CCM ijiandae kuzikabili changamoto zifuatazo:

(i) Kwanza Mheshimiwa Lowassa, yeye mwenyewe haonekani kama atayapokea matokeo hayo japo kwa shingo upande, bali upo uwezekano mkubwa wa kukubali “maombi” ya kujiunga na chama pinzani chenye nguvu ili agombee kupitia upinzani.

Na hapo ni lazima CCM “ijiandae” kupambana na nguvu kubwa ya upinzani ambayo itakuwa imeunganishwa na nguvu kutoka ndani ya CCM ya wale “CCM Lowassa” ambao watakuwa wamekasirishwa sana kutokana na “kuenguliwa” kipenzi chao, Mheshimiwa Edward Lowassa. Kwa mtazamo wa wafuasi hao, “Lowassa kwanza, CCM baadae”.

Japokuwa Wapinzani wamekuwa wakitamka hadharani mara kwa mara hawatohitaji “makapi” ya CCM, lakini kamwe tusijidanganye kwamba Wapinzani watadharau nguvu ya Mheshimiwa Lowassa katika kuwafanya Wapinzani wafungue ukurasa mpya wa kuiondoa CCM madarakani kwa kutumia nguvu ya mwana CCM huyo “mstaafu”.
 
Je, CCM wamejiandaa kukabiliana na nguvu hiyo ya Mheshimiwa Lowassa iliyounganishwa na nguvu ya vyama vya upinzani?

(ii) Jambo la pili ambalo CCM wanatakiwa wajiandae nalo baada ya “kumuengua” Mheshimiwa Lowassa katika kukiwakilisha chama kwenye kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao, ni namna ya kuishi na wana CCM ambao watakuwa ni “mamluki” wa Lowassa.

Na kwa kuwa watakuwa hawajulikani, wanaweza “kuvuruga” mbinu zote za ushindi za CCM na hatimaye CCM kushindwa au kushinda kwa ushindi “mwembamba” mno ili wawaonyeshe Watanzania umuhimu wa Lowassa.
 
Je, CCM imejiandaa vipi kulikabili kundi la wafuasi wa Lowassa ambao wamo ndani ya CCM? Je, ni vipi wataweka mbele maslahi ya CCM kwanza wakati mgombea wao Lowassa hakupita?

(iii) Jambo la tatu ambalo CCM wanapaswa kujiandaa kukabiliana nalo baada ya “kumkataa” Mheshimiwa Lowassa ni kitendo cha kunyimwa kura kwa mgombea wa CCM au kitendo cha wafuasi wa Mheshimiwa Lowassa kupeleka kura zao kwa mgombea wa Upinzani (hata kama atakuwa si Mheshimiwa Lowassa).

Wafuasi wa Lowassa watachukua uamuzi huo wa hasira kwani hata ukiwasikia baadhi yao hivi sasa, unaona wazi kwamba hawakujiandaa hata kidogo kushindwa bali wamejiandaa kushinda kwa asilimia mia moja.

CCM itapata wakati mgumu sana baada ya kumnyima Lowassa nafasi ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM kwani Mheshimiwa Lowassa ameshajijengea “mazingira” yanayoonyesha kwamba anapendwa sana na idadi kubwa ya Watanzania wakiwemo baadhi ya Masheikh waliothubutu kwenda kumuomba akubali kugombea cheo hicho cha urais.

Pia baadhi ya viongozi wa dini ya Kikristo ambao wamekwenda kumuomba agombee pamoja na kumfanyia “maombi” nyumbani kwake Dodoma. Wengine ni baadhi ya waendesha “bodaboda” pamoja na wajasiriamali kadhaa.

Kwa bahati mbaya sana, Mheshimiwa Lowassa bado hajawaambia wapenzi na wafuasi wake kwamba ili kura ya mwendesha bodaboda au mamalishe au kiongozi wa kidini iwe na thamani, ni lazima kwanza Kamati ya Maadili ya CCM, Kamati Kuu ya CCM, Halmashauri Kuu ya CCM na Mkutano Mkuu wa CCM; wajiridhishe kwamba Mheshimiwa Lowassa “anauzika” na anaweza kuongoza katika cheo hicho cha juu cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa ujumla, CCM ina mtihani mgumu sana katika kazi ya kuchuja wagombea na ni lazima ijiandae kwa faida na hasara kwa kila mgombea kutokana na kumkataa au kumkubali kwao.
 
Lakini kwa kuanzia tathmini hiyo, waanze na huyu Mheshimiwa Lowassa. Je, CCM imejiandaa vyema na changamoto za kumkataa au kumkubali Lowassa? Kama haijajiandaa, inapaswa iamke kutoka katika “usingizi mzito” na ifanye tahtmini hiyo sasa.

Changamoto ambazo CCM wanatakiwa kujiandaa nazo kwa kumkataa au kumkubali Mheshimiwa Lowassa zipo nyingi sana, cha msingi ni kuwakumbusha wana CCM kuwa makini kwani ni CCM pekee ndiyo inayoonekana kuwa kimbilio la Watanzania kwa nafasi ya mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baadhi ya Watanzania huwa wanajaribu kubadilisha vyama katika ngazi ya serikali za mitaa, udiwani na ubunge; lakini katika ngazi ya urais bado wanaiamini CCM kuwaletea kiongozi bora.
 
Kwa muktadha huo, CCM nayo inalazimika kujipima na kutafakari mapema yote yanayotarajiwa kujiri katika Uchaguzi kwani uchaguzi sio tukio la ghafla bali ni tukio linalojulikana mapema hivyo mipango ipangwe mapema pia.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. KAULI TUHUMA ZA KIPUUZI ZISITUNYIME RAIS BORAA ZIZINGATIWE TENA KWA HERUFI KUBWA

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad