Wachimbaji wadogo wa dhahabu mkoani Shinyanga, maarufu 'manyani', wamekufa katika machimbo madogo ya Kalole wilayani Kahama, baada ya kufukiwa na kifusi usiku wa kuamkia jana.Vifo hivyo vilitokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Akizungumza kwa simu, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya alisema wachimbaji hao walikumbwa na mauti hayo baada ya kuingia ndani ya mashimo hayo kwa njia ya panya kwa lengo la kutafuta mawe yenye dhahabu.
Mpesya alisema wachimbaji hao ni wale ambao huingia mashimoni kuiba mawe hayo, baada ya muda kumalizika wa kufanya kazi ambayo kwa kawaida huishia saa 12.00 jioni.
Baada ya hapo, imeelezwa ndio watu hao 'manyani' huvamia mashimo hayo nyakati za usiku kwa kuiba mawe hayo.
Katika tukio hilo, Mpesya alisema wachimbaji hao wote 19 waliingia kwenye mashimo manane, ambayo yameunganika kwa chini, walikufa baada ya mashimo hayo kuanza kubomoka kutokana na mvua hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema baada ya ajali hiyo, kazi ya kufukua ilifanyika ambapo maiti 19 waliopolewa ingawa kutokana na hali ya unyevu kwenye mashimo hayo yanayoendelea kutitia, wamelazimika kusimamisha ufukuaji.
“Unajua hawa ndugu zetu ni wale wachimbaji wasiokuwa na mashimo ambao muda ukiisha wa kazi huingia kwenye mashimo hayo bila kuangalia usalama na ndivyo ilivyotokea kwa wachimbaji hao,” alisema Mpesya na kuongeza kuwa maiti 17 kati 19 wametambuliwa na ndugu zao.
Katika jitihada za kutafuta wengine, tayari wameomba mashine za kufukua kutoka katika mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu pamoja na zile za kunyonya maji.
Mpesya alisema idadi inaweza kuongezeka baada ya kazi ya kufukua kukamilika kwa kuwa hawawezi kujua kama maiti hao 19 ndio hao hao waliokuwemo ndani ya mashimo hayo.
“Tunasubiri wenzetu kutoka mgodi wa Bulyanhulu waje waone kwanza mitambo ipi ambayo inaweza kutumika kufukua mashimo hayo, kwa kuwa ufukuaji wa kienyeji tuliokuwa tukiutumia tumeusimamisha kutokana na mashimo hayo kuendelea kutitia,” alisema Mpesya.
Machimbo hayo yako katika Kijiji cha Kalole katika Kata ya Lunguya katika Halmashauri ya Msalala. Ni moja ya migodi ya wachimbaji wadogo wanaokisiwa kufikia 30,000 na tayari wengi wao wamejipatia mamilioni ya fedha kwa uchimbaji huo wa kienyeji, ingawa hali hiyo ni hatari katika maisha yao wakati wa mvua za masika.