Moja ya maeneo ambayo katika siku za karibuni yamekuwa yakitoa ajira nyingi nchini na mataifa mengine ulimwenguni ni majeshi.
Wanawake ni sehemu ya wanaonufaika na ajira ya taasisi hiyo nyeti kwa nchi zote ulimwenguni, huku idadi yao ikitajwa kuongezeka kwa kasi katika kazi hizo za ulinzi wa mataifa yao huku swali kubwa likiwa je, wanawake hupata wakati mgumu zaidi ya wanaume jeshini?
Swali hilo linajibiwa na utafiti wa hivi karibuni unaobainisha kuwa taasisi hizo si rafiki kwa wanawake tofauti na ilivyo kwa wanajeshi wanaume.
Utafiti wa Taasisi ya Women’s Rights uliopewa jina la Changamoto zinazowakabili wanawake jeshini, unabainisha kuwa wengi wa wanawake walio jeshini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi kuliko wanaume.
Utafiti huo unaeleza kuwa wanawake wana wakati mgumu jeshini kutokana na kukumbwa na visa tofauti vya unyanyasaji vinavyowanyima haki.
Utafiti huo ambao uliakisi pia jinsi wanajeshi wa kike wanavyotumika wakati wa vita, unabainisha kuwa mara nyingi wanajeshi wanawake hutumika katika kazi za kutoa huduma na kuonekana kama ‘wauza sura’ wakati wanaume wakiwa mstari wa mbele, jambo ambalo linawapunguzia thamani ikilinganishwa na wanajeshi wanaume.
“Wanakabiliwa na changamoto nyingi kama vile talaka, ukosefu wa huduma bora za afya kulingana na jinsia zao. Pia, kubughudhiwa kimapenzi na visa vingine vya namna hiyo, ingawa wana umuhimu wa kipekee katika medani hiyo,” unabainisha utafiti huo.
Utafiti huo unasisitiza kuwa pamoja na changamoto zote wanazokabiliana nazo, wanawake wamekuwa na umuhimu wa kipekee.
Matokeo ya utafiti huo yametangazwa ikiwa ni wiki chache tangu Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Leon Panetta atangaze nia ya jeshi la nchi hiyo kurudisha mfumo liliouacha miongo miwili iliyopita wa wanawake kupelekwa mstari wa mbele jeshini.
Hatua hiyo imekuja huku nchini humo kukiwa na wastani wa matukio 19,000 ya mashambulizi ya kingono kwa wanajeshi wanawake kila mwaka.
Hata hivyo, hali hiyo inapuuzwa na Panetta, anayesema kuwa malengo ya idara ni kupata wanajeshi wazuri wenye sifa kwa ajili ya mstari wa mbele bila kujali jinsia.
“Wanawake wameonyesha ari na moyo mkubwa wa kujitolea,” anasema Panetta na kuongeza kuwa atahakikisha mpango huo wa kuwarudisha wanawake jeshini unawapata wenye sifa na weledi wa hali ya juu katika uwanja wa mapambano.
Anasema awali mpango huo ulishindikana kutokana na sera za nje za Marekani hasa baada ya kuingia katika vita nchini Afghanistan na kuonywa kuwa utekelezaji wa mpango huo utakuwa mgumu kwa wanawake kupelekwa vitani katika nchi hiyo.
‘Kuna ambao walipelekwa kwa ajili ya kuhudumu katika kambi zilizokuwa nchini Afghanistan na kuna ambao walipoteza maisha kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo maradhi ya kuambukiza.
Kuzuiwa kwa wanajeshi hao wa kike kulitokana na sababu nyingi, lakini baadhi ya wadadisi wa masuala ya kijeshi wanailaumu Pentagon kwa kutowajali askari wa kike, badala yake kutoa kipaumbele kwa wanaume.
“Pentagon ina utamaduni wa kutowajali askari wa kike ambao pia hawapewi fursa sawa na wenzao (wanaume), wanachukuliwa kama ni watu wa daraja la pili, wakiwa ni watu wa kuwastarehesha wengine kambini,” anasema Helen Benedict, mwandishi wa Kitabu ‘The lonely Soldier’ ambaye pia ni mwandishi wa habari na profesa katika Chuo Kikuu cha Columbia.
Anasema kukosa kuthaminiwa kwa wanawake wanajeshi ni tabia ya muda mrefu na huchangia udanganyifu katika utoaji wa taarifa za matukio ya mashambulizi kingono.
Anafafanua kuwa huo ni utamaduni utakaochukua muda mrefu kubadilika na kwamba kaulimbiu kuwa watu wote ni sawa, huenda ikabadili mtazamo.
“Naamini kunapokuwa na kundi la watu katika madarasa mawili tofauti, moja kwa ajili ya mashujaa na jingine kwa watu wa kundi jingine ni wazi kuwa unaelekea katika vitendo vya namna hiyo,” anasema Dempsey na kuongeza kuwa kadri watakavyowatendea kwa usawa, ndivyo nao watakavyotendeana.
Kauli ya JWTZ
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa JWTZ, Joseph Masanja alikataa kuzungumzia utafiti huo. “Siwezi kuzungumzia utafiti huo wala kueleza hali halisi ilivyo” alisema na kukata simu.
Hata hivyo, kimtazamo, wanawake hawaonekani kuwa na jukumu la kuwapo mstari wa mbele, ingawa baadhi ya nchi za Kiafrika zimekuwa na utaratibu kwa wanawake kushiriki vitani.
Sierra Leone kupitia azimio lililofikiwa nchini Ghana la Accra-based Women Peace Security (WISPEN) ni moja ya nchi ambazo wanajeshi wanawake hushiriki vitani na kuwa mstari wa mbele. Mpango huo unafadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Maendeleo kwa Wanawake (UNIFEM) ambao umefanya hivyo ili kuvunja mila na imani potofu zinazowabagua wanawake.
Shinikizo jingine la kufanya mapinduzi hayo ni kutokana na kuwapo kwa visa vingi baada ya ghasia za mwa 1991-200o zilizosababisha wanawake na wasichana wengi kubakwa na kudhalilishwa kijinsia na wanajeshi wa makundi yaliyokuwa hasimu.
Na wenyewe si wanataka haki sawa sasa malalamiko ya nini? Jeshi kwa mwanamke halifai,asili ya mwanamke sio ukakamavu.
ReplyDelete:) wakae nyumbani wapike tu ao na wasubiri kuwapokea waume zao wakitoka vitani(kazini) :))
ReplyDelete