Dkt. Hamisi Kigwangala acharuka, ataka wagombea urais wanaotumia fedha majina yao yakatwe

MBUNGE wa Jimbo la Nzega mkoani Tabora, Dkt. Khamis Kigwangala amekitahadharisha Chama cha Mapinduzi (CCM) kihakikishe hakiteui mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu atakayebainika kuusaka uongozi kwa kutumia fedha vinginevyo kitaanguka vibaya kwenye uchaguzi huo.

Dkt. Kigwangala ambaye ni mmoja wa wana CCM walioonesha nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM alitoa tahadhari hiyo alipokuwa akihutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Nzega na vitongoji vyake katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Parking mjini humo.


Alisema wakati Taifa likijipanga kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ni muhimu kwa CCM ikajipanga vizuri katika kupanga safu ya wagombea wake kuanzia ngazi zote za udiwani, ubunge na urais kwa kuhakikisha haisimamishi wale wote walioanza kusaka uongozi huo kwa kutumia fedha.

Alisema baadhi ya walioonesha nia ya kutaka kuteuliwa kugombea nafasi ya urais hivi sasa wanapitapita maeneo mbalimbali wakigawa fedha kwa wajumbe watakaohusika na vikao vya uteuzi ili waweze kuteuliwa hali ambayo alisema inapingana na tararibu na kanuni za CCM.

“Ndugu zangu binafsi naendelea kuwathibitishia kwamba nia yangu ya kutaka kugombea urais wa nchi ipo pale pale, na niwaeleze wazi kwamba sijatoa uamuzi kuhusu kugombea kwangu tena ubunge katika jimbo hili la Nzega, kwanza nimejikita kwenye urais, iwapo nitashindwa huko ndipo nitatoa uamuzi kama nitagombea ubunge au laa,”

“Hata hivyo napenda nitumie nafasi hii kukitahadharisha Chama changu cha CCM kiwe makini katika uteuzi wa mgombea wake katika nafasi hii nyeti ya urais wa Jamhuri ya Muungano, isifanye kosa hata kidogo kwa kumteua mtu ye yote ambaye tayari ameonesha dhahiri kuusaka urais kwa kutumia fedha,”

“Tunataka CCM isimamishe mgombea aliye safi asiye na doa lolote au kashifa yoyote ya ufisadi katika nchi hii, bali izingatie mtu mwenye agenda na anayeeleza iwapo atachaguliwa kuwa rais atawatendea kitu gani watanzania, siyo sifa ya kuwa na fedha nyingi, nyingine tunajua zimeibwa kutoka serikalini, hii hatukubali,” alieleza Dkt. Kigwangala.

Alisema yeye binafsi anaamini CCM itahakikisha hakuna mgombea ye yote ambaye amebainika tayari anakwenda kinyume cha kanuni na maadili ya chama na ambao hivi sasa wanapitapita kwa wajumbe wa vikao vya uteuzi wakimwaga fedha atakayeteuliwa bali majina yao yote yatakatwa mapema.

Akifafanua Dkt. Kigwangala alisema iwapo CCM itamsimamisha mgombea ye yote mwenye dosari na aliyebainika kutumia fedha katika kuusaka uongozi ni wazi watanzania watahoji maana wengi sasa ni wajanja na wana akili, ni vigezo vipi vilivyotumika kumteua maana CCM daima inaimba rushwa ni adui wa haki, sasa lazima ioneshe kwa vitendo jinsi inavyoichukia rushwa.

“Hawa wanaotumia fedha mpaka hivi sasa hawajaweza kuwaeleza wananchi iwapo watachaguliwa watawafanyia nini, binafsi mimi nina agenda na hoja ya kwa nini nataka kugombea urais, na nimeandikika kitabu kueleza nitakayoyafanya, naamini wengine walioonesha nia ni dhaifu sana, hawana agenda yoyote ya maana mbali ya kuegemea kwenye uwezo wao wa kifedha,”

“Hata chama changu cha CCM hakiamini katika watu wanaotumia fedha, kanuni zetu zikiheshimiwa katika vikao vya awali, majina ya wengi wao yatakatwa hata kabla ya kufikishwa kwenye vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri kuu ya Taifa (NEC), na wengi mtashangaa maana majina yatakayojitokeza ni ya wagombea vijana,” alieleza Dkt. Kigwangala.

Aidha mbunge huyo alisema itakuwa ni ajabu kwa vikao vya uteuzi ndani ya CCM kuteua mgombea ambaye atasababisha wananchi kuwa na maswali mengi juu yake wakati wa kipindi cha kampeni mfano wa wale ambao awali walitakiwa kuvuliwa magamba lakini baadae yaliishia mabegani na wakasafishwa kwa kusamehewa.

“Wapo waliotakiwa kuvuliwa magamba, wanafahamika, leo hii itokee CCM iwasimamishe kama wagombea itakuwa ajabu kubwa, sijui mtu atasimamaje jukwaani kuwanadi, lazima wananchi watahoji hawa wamekuwa wasafi lini? baadhi yao fedha walizonazo walizipata kupitia madaraka waliyokuwa nayo serikalini, leo tena waletwe kwenu eti ndiyo wagombea urais wa CCM, hapana litakuwa ni jambo la kushangaza sana,” alieleza.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad