Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari wa Sekretarieti kwenye Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi mjini Dodoma leo tarehe 22 Mei 2015.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamati Kuu imepokea na kutafakari taarifa ya Kamati ya Usalama na Maadili ambayo ilipitia adhabu waliyopewa wanachama sita waliokiuka kanuni za Maadili na kupewa Onyo Kali, adhabu iliyodumu kwa kipindi kisichopungua miezi 12.
Wanachama hao sita ni;-
i. January Makamba
ii. Willium Ngeleja
iii. Steven Wasira
iv. Bernard Membe
v. Edward Lowassa
vi. Fredrick Sumaye
Kamati Kuu imepokea na kukubali pendekezo la Kamati ya Usalama na Maadili ya kumalizaka kwa kipindi cha adhabu kwa wanachama hawa. Kwahiyo adhabu hiyo kwa sasa imemalizika, na wanachama hao wameruhusiwa kuendelea na shughuli zao katika Chama.
Hata hivyo Kamati Kuu inawataka wanachama hawa na wale wengine wenye nia ya kugombea Urais kupitia CCM Kuzisoma , Kuziheshimu na Kuzizingatia Kanuni za Maadili za CCM na kanuni zingine zinazoongoza mchakato ndani ya Chama, ili wasikumbwe na adhabu itokanayo na kuzivunja kanuni hizo.
Wale wote wanaotaka kugombea, yaani waliokuwa kwenye adhabu na wengine watakaojiingiza kwenye kampeni mapema na hivyo kukiuka maadili na miiko ya Chama, taarifa za kukiuka kwao zitatumiwa wakati wa kuchuja majina ya wagombea utakapofika.
Taarifa hizo zitatumika katika kuwapima na kuamua iwapo wana sifa za kutosha na wanafaa au hawafai katika kupata uteuzi wa nafasi wanayoiomba.
Imetolewa na;-
Nape Moses Nnauye
Katibu wa Itikadi na Uenezi
22/05/2015