Serikali ya Burundi imewataka waandamanaji katika mji mkuu wa Burundi Bujumbura kusitisha maandamano yao dhidi ya hatua ya rais wa taifa hilo Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu katika uchaguzi wa mwezi ujao.
Serikali imewapatia waandamanaji hao saa 48 kuondoa vizuizi walivyoweka katika barabara za mji huo,lakini hata hivyo inadaiwa maandamano yataendelea leo siku ya jumapili.
Wanasiasa wanasema kuwa bwana Nkurunziza anakiuka katiba kwa kuwania muhula wa tatu,lakini mapema wiki hii mahakama ya kikatiba nchini Burundi iliamua kuwa rais Nkurunziza ana haki ya kuwania muhula wa tatu.
Hadi sasa takriban watu 18 wameuawa tangu maandamano hayo yaanze wiki mbili zilizopita.