Rais Kikwete Awatolea Uvivu Vijana wa CCM.....Awataka Waache Ukuwadi

RAIS Jakaya Kikwete, amesema Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umegeuka kuwa jukwaa la watu wanaotaka kugombea urais kwa kuwa makuwadi, mawakala wa kuhonga fedha vijana wenzao badala ya kufanya mijadala ya kukijenga chama.

Alisema lazima vijana wa UVCCM wawe wapiganaji, wapambanaji na wanaharakati wa kukiimarisha chama kwani hatima ya CCM iko mikononi mwao.

Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, aliyasema hayo Mjini Dodoma jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu nchini.

Alisema badala ya umoja huo kukaa na kuzungumza mambo ya mustakabali wa chama na Taifa, baadhi ya viongozi wake huchukua fedha kwa wazee na kuwagawia vijana.

"Vijana hampaswi kuwa makuwadi na mawakala wa kuhonga wenzenu, katika Kikao cha NEC, nilimuita Sixtus Mapunda (Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa) na wenzake nikamwambia mnakoenda siko rudini huku...sisi tunategemea miaka 30 ijayo Rais atoke miongoni mwenu hivyo lazima tufanye kazi ya kuwaandaa vijana ili wawe viongozi wazuri.

"Utakuta viongozi wanasafirishwa ili kuwasindikiza wazee wanaotaka urais jambo ambalo haliwezekani vijana kuhusishwa na ugawaji rushwa, enzi zetu hoja za vijana zilikuwa zina nguvu lakini sasa hivi vijana si tishio tena," alisema.

Aliongeza kuwa, hivi sasa vijana hawatoi hoja za kukijenga chama hivyo aliwataka warudishe misingi ya uanzishwaji wake na kusisitiza kuwa, anaamini shirikisho hilo litakipa uhai CCM na kutoa mawazo ya kujenga chama.

Rais Kikwete alisema, jukumu la shirikisho hilo ni kukitafutia chama wanachama, marafiki na kuhakikisha kinaungwa mkono na wanafunzi wa elimu ya juu na wengine.

"Shirikisho hili lina wajibu wa kuwa chombo cha uwakilishi wa masilahi ya wanafunzi, kuwa wepesi kuyatambua mambo yenye masilahi kwa wanafunzi na kuyasemea.

"Muwe tumaini na kimbilio la wanafunzi, tatueni changamoto na kuzisemea kwa chama na Serikali badala ya kuacha mambo yakaharibika...shirikisho hili ni tanuru la kupika viongozi wa baadaye hivyo lazima muwe na mipango madhubuti," alisema.

Aliwataka kuchagua viongozi wazuri, waaminifu, waadilifu, wabunifu na wachapa kazi ndani ya shirikisho ambao watakuwa na uwezo wa kujenga hoja.

"Chama kinasema jitokezeni kugombea, nasubiri hiyo Juni 3, mwaka huu nione watajitokeza wangapi maana ninavyosikia
wako wengi zaidi ya 20 wanaotaka urais.

"Lazima tushirikiane kujenga chama chetu na shirikisho, mimi nilijaribu mwaka 1995 kugombea urais lakini kura hazikutosha na sikumnunia Mzee Mkapa," alisema Rais Kikwete.

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, mlezi wa shirikisho hilo Bw.January Makamba, alisema shirikisho lina matawi 137 katika mikoa mbalimbali nchini ambapo changamoto zinazowakabili vijana ni mikopo ya wanafunzi, ushirikishwaji katika kampeni na suala la ajira hivyo alimwomba Rais Kikwete kuyatafutia ufumbuzi.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. A LOST NATION INTO DEEP DEEPLY DARKNESS

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad