Sakata la Escrow: IKULU Yasema Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini Ndugu Eliakim C. Maswi Hana HATIA

MATOKEO YA UCHUNGUZI WA AWALI KUMHUSU NDUGU ELIAKIM C. MASWI, KATIBU MKUU, WIZARA YA NISHATI NA MADINI
_________________________________________________

1.0    Utangulizi

1.1  Katika mkutano wake wa 16 na 17, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na mambo mengine, lilijadili Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali iliyotokana na Taarifa ya Ukaguzi wa Akaunti ya Tegeta Escrow uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

1.2 Baada ya majadiliano, Bunge lilipitisha maazimio kadhaa yaliyoelekezwa kwa Serikali kwa ushauri na utekelezaji.
 
Mojawapo ya maazimio hayo yalimtaja Ndugu Eliakim C. Maswi, ambaye ndiye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kuwa amehusika kijinai au kimaadili katika miamala iliyotokea katika akaunti ya Tegeta Escrow.

1.3 Wakati anahutubia Taifa kupitia Wazee wa Dar es Salaam tarehe 22 Desemba, 2014, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema ifuatavyo:-

“Kuhusu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni Mtumishi wa Umma, anatawaliwa na Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma. Hivyo, nimeshaelekeza Mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye ikibainika ana makosa hatua za kinidhamu zitachukuliwa.”

1.4 Tuhuma dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi zimeshughulikiwa katika ngazi mbili tofauti. Amechunguzwa na Sekretarieti ya Maadili ya Umma, kisha baada ya hapo alichunguzwa pia na Kamati ya Uchunguzi wa Awali iliyoundwa na mamlaka yake ya nidhamu.

2.0    Sekretarieti ya Tume ya Maadili

2.1 Kifungu 18 (2) (c) na (3) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kinaipa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma mamlaka na uwezo wa kuchunguza tuhuma yoyote ya kuvunjwa kwa maadili ya uongozi wa umma yanayotawaliwa na Sheria hiyo. 
 
Tuhuma dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi zilizomo kwenye maazimio ya Bunge zinatawaliwa na Sheria hiyo.

2.2 Katika kutekeleza majukumu yake, Sekretarieti ya Maadili ya Umma ilifanya uchunguzi wa awali na kisha kumhoji Ndugu Eliakim C. Maswi tarehe 19 Desemba, 2014.

2.3 Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma haijabaini kuwepo kwa maslahi binafsi katika uamuzi uliofanywa na Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini wa kuruhusu fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow kutolewa. 
 
Aidha, hawakubaini ukiukwaji wowote wa maadili ya viongozi wa umma uliofanywa na Ndugu Eliakim C. Maswi. 
 
Waliona kuwa yote aliyoyafanya yalizingatia matakwa ya Sheria, ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na ridhaa ya TANESCO. Hivyo, Sekretarieti ya Maadili haikuona msingi wowote wa kuendelea na shauri la Ndugu Eliakim C. Maswi, na wamelihitimisha.

3.0 Kamati ya Uchunguzi wa Awali ya Mamlaka ya Nidhamu

3.1 Kwa mujibu wa Kifungu 4(3) (d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 (kama ilivyorekebishwa) Katibu Mkuu Kiongozi ndiye Mamlaka ya Nidhamu ya Makatibu Wakuu.

3.2 Kwa kuzingatia Azimio husika la Bunge, na kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katibu Mkuu Kiongozi aliunda Kamati ya Uchunguzi wa Awali dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, chini ya Kifungu cha 36 cha Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003 kinachotamka ifuatavyo:-
 
“Where it is necessary to institute disciplinary proceedings against a public servant, the disciplinary authority shall make preliminary investigations before instituting disciplinary proceedings.”

3.3    Kwa mamlaka aliyonayo chini ya Kanuni 35(2)(b) na Kanuni 37 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, Katibu Mkuu Kiongozi alimpumzisha Bwana Eliakim C. MASWI kutekeleza majukumu yake ya kazi ya Katibu Mkuu ili kupisha uchunguzi wa awali. 
 
Uchunguzi wa awali ulifanyika chini ya Kanuni ya 36 ya Kanuni za Utumishi wa Umma zilizotajwa, pamoja na Kifungu 4(3) (d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002, kama ilivyorekebishwa.

3.4 Kwa mamlaka aliyonayo chini ya Kanuni zilizotajwa kwenye ibara 3.3 hapo juu, Katibu Mkuu Kiongozi aliteua Kamati ya Uchunguzi wa Awali na kuipa Hadidu za Rejea zifuatazo:

3.4.1 Kubainisha wajibu na madaraka halisi ya Katibu Mkuu, Wizaraya Nishati na Madini, kwenye uendeshaji wa TANESCO kwa ujumla, na hususan kwenye kufungua, kuendesha na hatimaye kufungwa kwa akaunti ya Tegeta Escrow.

3.4.2 Kubainisha na kupata maelezo ya kina juu ya kuhusika kwa Bwana Eliakim C. Maswi katika mchakato na mtiririko mzima wa akaunti ya Tegeta Escrow, tangu kufunguliwa hadi kufungwa.

3.4.3 Kubainisha na kupata maelezo ya kina iwapo kuna jambo lolote ambalo Bwana Eliakim C. Maswi alilifanya au ambalo alipaswa  kulifanya lakini hakulifanya, linalomstahilisha achukuliwe hatua za nidhamu.

3.4.4  Kubainisha na kupata maelezo ya kina iwapo katika hatua yoyote ya mchakato na mtiririko wa tangu kufunguliwa hadi kufungwa kwa akaunti ya Tegeta Escrow, Bwana Eliakim C. Maswi alifanya  jambo lolote linalodhihirisha matumizi mabaya ya mamlaka yake kama Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa namna iliyosababisha hasara ya aina yoyote ile kwa Taifa la Tanzania.

3.4.5  Kubainisha na kupata maelezo ya kina iwapo katika hatua yoyote tangu akaunti ya Tegeta Escrow ilipofunguliwa hadi ilipofungwa, Bwana Eliakim C. Maswi hakuchukua tahadhari ya kutosha kulinda maslahi ya umma na kusababisha kupotea kwa fedha za umma kwa uzembe au matumizi mabaya ya madaraka.

3.4.6 Kubainisha iwapo kuna mahali popote katika mchakato wa akaunti ya Tegeta Escrow ambapo Bwana Eliakim Chacha Maswi alifanya jambo lolote linaloashiria kitendo cha kijinai, au kukiuka maadili ya viongozi wa umma.

3.4.7 Kuandaa taarifa ya uchunguzi wa awali kwa msingi wa Hadidu za Rejea zilizomo humu na kuiwasilisha kwa Katibu Mkuu Kiongozi. Taarifa hiyo, pamoja na mambo mengine, ipendekeze hatua za kuchukuliwa kwa kila eneo ambalo Kamati itabaini umuhimu wa hatua kuchukuliwa.

3.5   Mapendekezo ya Kamati ya Uchunguzi wa Awali

3.5.5 Kamati haijabaini kosa lolote ambalo linaweza kusababisha Ndugu Eliakim Chacha Maswi, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, kufunguliwa mashtaka ya kinidhamu kwa kukiuka Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 ikisomwa pamoja na Kanuni zake za mwaka 2003 kwa kuruhusu Benki Kuu ya Tanzania kutoa fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow.

4    Hitimisho la Uchunguzi wa Awali

4.4 Uchunguzi wa Awali uliofanywa na Sekretarieti ya Maadili umebaini kuwa Ndugu Eliakim C. Maswi hana makosa yoyote ya kimaadili katika mchakato wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow.

4.5  Hali Kadhalika Uchunguzi wa Awali uliofanywa na Kamati ya Uchunguzi wa Awali iliyoundwa na Katibu Mkuu Kiongozi umebaini kuwa Ndugu Eliakim C. Maswi, “hakutenda au kuhusika na jambo lolote linaloashiria vitendo vya jinai au kukiuka Maadili ya Viongozi wa Umma”.

4.6   Ushahidi wa vielelezo uliotolewa kwenye Sekretarieti ya Maadili na kwenye Kamati ya Uchunguzi wa Awali umejitosheleza kuthibitisha kwamba Ndugu Eliakim C. Maswi alitenda kazi yake kwa kiwango kinachoridhisha kwa kufanya mawasiliano na mamlaka mbalimbali na kwa nyakati tofauti kwa lengo la kuhakikisha na kujiridhisha kwamba kufungwa kwa Akaunti ya Tegeta Escrow kunafanyika kwa usahihi.

4.7 Hakuna ushahidi wowote kuwa Ndugu Eliakim C. Maswi alikuwa miongoni mwa waliopata mgao wa fedha au fadhila yoyote kutokana na kufungwa Akaunti ya Tegeta Escrow.

4.8 Kwa nafasi yake ya mamlaka ya nidhamu Katibu Mkuu Kiongozi, ameridhika kuwa Ndugu Eliakim C. Maswi hana makosa yoyote aliyoyafanya katika mchakato wa akaunti ya Tegeta Escrow yanayostahili adhabu. 
 
Hivyo, mchakato wa kinidhamu, kimaadili na kijinai dhidi yake umefikia mwisho wake. Mwenye mamlaka ya uteuzi atatafakari taarifa hizi na kuamua cha kufanya kuhusu ajira yake baadaye.
 
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
8 Mei, 2015

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad