WABUNGE wameishauri serikali kulipa deni la makandarasi wanaoidai Wizara ya Ujenzi linalozidi Sh. bilioni 850 kuwezesha bajeti iliyotengwa kufanya kazi za maendeleo.
Hayo yalitokea jana bungeni mjini Dodoma wakati wabunge hao wakichangia bajeti ya wizara hiyo ya takriban Sh. bilioni 900.
Akisoma hatuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR Mageuzi), alisema fedha iliyotengwa kwa ajili ya maendeleo katika wizara hiyo ni ndogo.
Alisema ujenzi ni sekta ambayo kibajeti inachukua asilimia kubwa, lakini kiuhalisia ina madeni makubwa kutoka kwa makandarasi na washauri.
“Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alisema kipo kikosi kazi cha kuhakiki madeni ya wazabuni kwa wizara mbalimbali. Moja ya wizara hizo ni hii ya ujenzi.
“Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, kueleza kikosi kazi kilichoundwa kuhakiki uhalali wa madeni ya wizara kimebaini ni kiasi gani kinachodaiwa,” alisema Mkosamali.
Alisema wizara hiyo hadi sasa inadaiwa Sh. biloni 800 na hakuna majibu ya namna yatakavyolipwa pamoja na mbwembwe za uwasilishwaji wa Bajeti ya Wizara ya Ujenzi.
“Pamoja na kelele na mbwembwe nyingi, ukweli ni kwamba madeni ya wizara yanazidi fedha za maendeleo tunazopitisha bungeni,” alisema.
Alisema mwaka 2014/2015, madeni ya wizara hiyo yalikuwa Sh. bilioni 760 huku bajeti ya maendeleo ikiwa ni Sh. bilioni 762.
“Ni dhahiri kuwa wizara haikuwa na fedha za maendeleo kwa mwaka huo wa fedha. Hivyo waziri alieleze ukweli Bunge kwenye Bajeti hiyo ni fedha kiasi gani zimelipa madeni?” alihoji.
Mkosamali alisema zipo taarifa kwamba makandarasi watatu wamekufa kutokana na msongo wa mawazo baada ya serikali kutowalipa madeni yao walipomaliza kazi.
Akizungumzia ununuzi wa kivuko cha Bagamoyo, Mkosamali alisema kilinunuliwa kwa shilingi bilioni nane, kinabeba abiria 300 huku kikitumia saa tatu kutoka Dar es Salaam hadi Bagamoyo.
“Ni jambo la ajabu kununua kivuko cha kizamani, chakavu chenye spidi ndogo. Bakhresa ana meli inayotoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kwa dakika 90 tu ikiwa na abiria 500 na taarifa tulizonazo, bei yake ni kati ya Sh. bilioni 4 na 5 tu.
“Tunaomba Bunge kuunda Tume itakayochunguza ununuzi wa kivuko hiki kibovu na cha kizamani kilichonunuliwa kwa bei kubwa huku kikienda mara moja tu Bagamoyo kwa siku,” alisema Mkosamali.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema serikali imeshindwa kutatua kero ya foleni jijini Dar es Salaam pamoja na majiji mengine makubwa na kwamba juhudi za makusudi zinapaswa kufanyika kunusuru wananchi wa miji hiyo.
Awali akiwasilisha Bajeti ya Wizara hiyo, Dk. Magufuli alisema fedha walizoomba ni zaidi ya Sh. bilioni 900 zitakazosaidia maendeleo ya kuboresha barabara, madaraja na vivuko katika maeneo mbalimbali.