Wenye "Homa Ya Lowassa" Wanayapuuza Ya CAG Wanang'ang'ania Ya Richmond Wakiamini Ndo Njia Pekee Ya Kumharibia

Kwa  nini  sakata  la  Ufujaji  umeme  wa  dharura  la  kampuni  ya  Richmond  liliolazimu  kupangwa  upya  baraza  la  mawaziri  linazungumzwa  kwa  nafasi  kubwa  na  wanasiasa  hadi  sasa, huku  ripoti  ya  mdhibiti  na  mkaguzi  mkuu  wa  hesabu  za  Serikali-CAG  zinazoibua  ubadhirifu  mkubwa  kila  mwaka  zikisahaulika  kirahisi?


Kama  waziri  mkuu  mstaafu  Edward  Lowassa  asingehusishwa  na  sakata  la  Richmond  kwa  namna  washindani  wake  kisiasa  wanavyolazimisha, sakata  lingeendelea  kuzungumzwa?

Maswali  haya  mawili  yana majibu  yake  sahihi  kwa  wanaojua  undani  wake, akiwemo  Lowassa  aliyejiuzulu  ili  kulinda  heshima  na  mustabali  wa  nchi, serikali  na  chama  cha  mapinduzi-CCM, kama  anavyonukuliwa  akisema. Yawezekana  amelinda  maslahi  ya  nchi  kwa  vile  wahisani  hawakusitisha  misaada  yao  muhimu  kwa  bajeti  ya  nchi.

Kwa  muktadha  wa  makala  na  ulinganifu  wenye  mantiki,  hakuna  manufaa  makubwa  kwa  umma  kupigia  kelele  Richmond  iliyopitia  Dowans  na  kubaki  Symbion Power  na  kujisahalisha  huu  ubadhirifu  na  upotevu  mkubwa  wa  fedha  za  umma  unaobainishwa  kila  mwaka  na  CAG  bila  kufanyiwa  kazi  ipasavyo  kwa  hatua  stahiki  dhidi  ya  wahusika.

Hizi  mbinu  za  kisiasa  za  kukumbuka  Richmond  ili  kutimiza  malengo  ya  baadhi  ya  wanasiasa  ya  kulazimisha  na  kuwaaminisha  watu  mambo  yawe  watakavyo  yanazidi  kufifia  na  kushindwa  kadri  siku  zinavyozidi  kubadilika.

Eti  wanakumbuka  sana  Richmond  kwa  vile  imehusishwa  na Lowassa!!!

Sina  nia  ya  kumsafisha  mchafu  yeyote  wala  kumchafua  msafi  bali  nauzungumzia  uhalisia  tu.Unawezaje  kukumbuka  Richmond  na  kukataa  kuona  ubadhirifu  unaoibuliwa  na  CAG  anapoonyesha  zaidi  ya  sh. trion moja  zimeyeyuka  serikalini?!

Kama  ilivyokuwa  Richmond  na waliouaminisha  umma  iwe  watakavyo  katika  bunge  la  kasi  na  viwango  la  Spika  Smweli Sitta  ndivyo  ilivyotokea  kwa  sakata  la  Tegeta  Escrow  ambapo  wanasiasa  wamethubutu  kutoa  hukumu  wanayolazimisha  iwe  dhidi  ya  wale  walioitwa  mafisadi, na  kuimiminisha  dhana  husika  kwa  wananchi.

Baadhi  ya  wahusika waliojiuzulu  kutokana  na  sakata  la  Esrow  kama  njia  ya  kuonyesha  uwajibikaji  kisiasa  wamethibitika  kutohusika. Kati  yao  ni aliyekuwa  waziri  wa  nishati  na  madini Profesa  Sospeter  Muhongo  na  katibu  mkuu  wake  Eliakim Maswi, ambao  kamati  maalumu  iliyoundwa  kuchunguza  uhusika  wao  haikuona  hatia  yoyote  dhidi  yao.

Bahati  mbaya, enzi  za  Richmond  hakukuwa  na  kamati  maalumu  ambayo  ingethibitisha, kwa  mfano, usafi  wa  wanasiasa  waliohusishwa  na  Richmond  baada  ya  kujiuzulu  kwao.

Sijui  wanasiasa  wanaoshupalia  Richmond  wakidhani  kuikumbuka  kwa  kutaathiri  safari  ya  kisiasa  ya Lowassa  wakiambiwa  ukweli  tofauti  watatumia  kete  gani  mpya  kujipandisha  kisiasa.

Wanasiasa  wenye  "homa  ya  Lowassa"  wanaamini  kete  pekee  ya  kufifisha  umaarufu, kukubalika  na  safari  ya  matumaini  ya  Lowassa  ni  kutumia  sakata  la  Richmond.

Bahati  mbaya  ya  makusudi  kwao  ni  kutowaambia  wananchi  ile  Richmond  wanayojikumbusha  hasa  kipindi  hiki  cha  kuelekea  uchaguzi  mkuu  octoba  mwaka  huu, ndiyo  hii Symbion  ambayo  Rais  wa  Marekani  Barack  Obama  anaijua  na  anaamini  kazi  inayofanywa  nayo  ndani  ya  Tanzania  katika  sekta  ya  Nishati.

Sasa  wewe  mwanasiasa  ukiikumbuka  Richmond, unganisha  Dowans  ili  uiseme  Symbion  kwa  sauti  ya  juu  itakayowafikia  wananchi  ili  waweze  kukuuliza  umefanya  nini  au  unakumbuka  yapi  angalau  kimya kimya  kuhusu  EPA,Kagoda,Meremeta,Deep Green Finance,Tegeta  Escrow; unachukuliaje  ripoti  mpya  ya  CAG  na  uamuzi  wa  wahisani  kusitisha  misaada  muhimu  ya  kibajeti  kwa  nchi.

Hadi  sasa  kunawatu  hawako  tayari  kusikia  tofauti  na  walivyoaminisha  au  kuaminishwa  juu  ya  Richmond.

Pengine  ule  msemo  apendao  kuutumia  Rais  Kikwete  kwamba  "Akili  za  kuambiwa  changanya  na  za  kwako"  ni  muafaka  kuwagutusha  watu  ili  wapambanue  dhamira  za  wanasiasa  kabla, wakati  na  baada  ya  kusikia  wanenacho  na  watendacho.

Endapo  wanasiasa  watadhani siasa  za  kuchafua  wagombea  wanaotakiwa  na  wananchi  walio  wengi  ili  wao  wasiotakiwa  wabahatike  kuteuliwa  na  vyama, yaliyomtokea  Goodluck  Jonathan  na  kilichokuwa  chama  tawala  Nigeria  si  ajabu  kujirudia  kwa  CCM.

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Siasa ya bongo michosho kinoma

    ReplyDelete
  2. Wewe na wao wote mnatuhumiwa kwa ufisadi, huwezi kujitetea kwa kupita taa nyekundu barabarani wa kusema mbona kuna mwengine wamepita hamwafuatilii kuwakamata jibu kosa lako.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad