Kituko Sakata la Mama Mjamzito Aliyejifungulia Bafuni baada Ya Wauguzi Kumfukuza

SIKU mbili baada ya tukio la wauguzi wawili wa zahanati iliyopo Kijiji cha Shishiyu, Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu kudaiwa kumfukuza mama mjamzito aliyejifungulia bafuni katika nyumba iliyopo jirani na zahanati hiyo, uongozi wa halmashauri hiyo umewahamisha kituo cha kazi wauguzi hao badala ya kuwachukulia hatua.

Wauguzi hao (majina yanahifadhiwa), wanadaiwa kumfukuza mama aliyekuwa mjamzito Rotha Bujiku baada ya kufika katika zahanati hiyo ili aweze kupatiwa huduma ya kujifungua.

Akizungumza na waandishi wa habari juu ya hatua ambazo zimechukuliwa kwa wauguzi hao, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Trasiasi Kagenzi, alisema wauguzi hao wamehamishwa kituo cha kazi na kupelekwa katika kituo kingine.

Alisema uongozi wa halmashauri umeona kabla ya kuwachukulia hatua za kinidhamu, uwahamishe kituo ili kuokoa maisha yao kwa kuwa wakazi wa kijiji hicho walikuwa wanataka kuwadhuru.

Aliongeza kuwa, hawakuona haja ya kuanza kuwachukulia hatua za kisheria wakati maisha yao yapo hatarini hivyo wamewanusuru kwanza na baadaye watachukuliwa hatua za kinidhamu.

"Suala la kuwahamisha na kuwachukulia hatua za kinidhamu ni vitu viwili tofauti...tukumbuke kuwa, kumchukulia mtumishi wa umma hatua za kinidhamu kuna taratibu zake.

"Kutokana na hali hiyo, tumeona hatua ya awali ni kuwatoa katika zahanati hii kwa sababu wananchi walitaka kuwadhuru kwa kitendo walichokifanya," alisema Kagenzi.

Alisema uongozi ulikaa na kutafakari kwa kina wakaona kuna haja ya kunusuru maisha ya wauguzi hao wakati utaratibu wa kuwachukulia hatua za kinidhamu ukiendelea na kuwahamisha kituo cha kazi hakizuii wasichukuliwe hatua.

Kagenzi alisema watumishi hao watachukuliwa hatua za kisheria baada ya uchunguzi kufanyika na kusisitiza kuwa, afya ya mama huyo na mtoto wake zinaendelea vizuri, huduma katika zanahati hiyo pia zinaendelea baada ya kupelekwa wauguzi wengine.

Aliongeza kuwa, wauguzi hao wamepelekwa katika vituo viwili tofauti ambapo mmoja kapelekwa Kituo cha Mwasayi kilichopo Kata ya Masanmwa, mwingine kapelekwa Zahanati ya Magereza Malya iliyopo Kata ya Buzinza na Mganga Mfawidhi amepelekwa Zahanati ya Bugalama ambazo zote zipo wilayani humo.

Wauguzi hao walifanya tukio hilo juzi kwa kile kilichodaiwa mama huyo walishampa maelezo ya kwenda kujifungulia katika Hospitali ya Wilaya hiyo kutokana na kujifungua mfululizo ambapo alikuwa amekwenda kujifungua mtoto wa 11.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad