Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana alisema kuwa muda wa mabadiliko aliyotabiri Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ni sasa na kwamba yeye ndiye anayeweza kuyaongoza.
Wakati Lowassa akisema hayo mjini Iringa, kada mwingine anayewania urais kwa kupitia chama hicho, William Ngeleja alikuwa mkoani Mwanza ambako alisema kuwa ana dhamira ya dhati na nia ya kuleta mabadiliko kwa maisha ya Watanzania.
Mjini Iringa, Lowassa alisema kuwa kwa sasa CCM inahitaji mabadiliko makubwa na akanukuu kauli ya Mwalimu Nyerere aliyoitoa mwaka 1995 alipozungumzia haja ya chama hicho kujisahihisha.
“Baba wa Taifa alisema kuwa Watanzania wanahitaji mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM,” alisema mbunge huyo wa Monduli kwenye hafla hiyo iliyofanyika Uwanja wa Samora mjini Iringa.
“Huu ni wakati wa mabadiliko. CCM ikijipanga inaweza kuleta mabadiliko na mtu wa kuleta mabadiliko hayo ni mimi,” alisema.
Lowassa alisema aliamua kuingia kwenye mbio za urais kwa sababu tatu, ambazo ni kufanya mabadiliko ndani ya CCM, kufanyia kazi tatizo la umaskini na kushughulikia tatizo la ajira kwa vijana.