WAKATI makada watano wakiwa wamejitokeza kutangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya chama tawala, CCM, leo ni zamu ya Waziri wa Nishati na Madini aliyejiuzulu, Profesa Sospter Muhongo.
Kwa mujibu wa kambi ya mwanajiolojia huyo maarufu duniani, atatangaza dhamira yake hiyo akiwa katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) Tawi la Musoma mkoani Mara.
Muhongo aliyejipatia umaarufu mkubwa wa uchapaji kazi akiwa waziri, anatajwa kujielekeza zaidi katika kuiweka Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati, hasa kwa kutumia rasilimali ya nishati ya gesi iliyogunduliwa nchini.
Kiongozi huyo ambaye kwa sasa amebaki na kofia yake ya mbunge wa kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, aliachia ngazi hivi karibuni kutokana na sakata la Escrow.
Hata hivyo, tume zilizoundwa kuchunguza sakata hilo, zilimsafisha yeye na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi.
Muhongo anatarajiwa kuungana na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Kilimo, Chakula la Ushirika, Stephen Wassira, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu) Profesa Mark Mwandosya na Mbunge wa Afrika Mashariki, Charles Makongoro Nyerere waliotangaza nia.
Kesho itakuwa zamu ya Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja. Ngeleja anatarajiwa kutangaza nia jijini Mwanza.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani anatarajiwa kutangaza nia wakati wowote wiki hii. Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe anatarajiwa kutangaza nia kijijini kwake Rondo mkoani Lindi Jumamosi wiki hii.
Akizungumza wakati wa Tamasha la Kaswida jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Membe aliyekuwa mgeni rasmi siku hiyo alithibitisha kutaka kutangaza nia hiyo na kuwaomba wananchi wamsikilize kwa makini siku hiyo, kwa kuwa ataeleza kwa kina nini anataka kufanya nchi iweze kuondoka ilipo na kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo.
Profesa Muhongo Nae Kutangaza Nia Ya Kuwania Urais LEO
0
June 02, 2015
Tags