SHULE ya Msingi Saadani Chumvi iliyopo Kata ya Mkange wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, imefungwa baada ya wazazi kuwa na hofu baada ya watu wawili na mbuzi 70 kuliwa na Simba kutoka kwenye Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
Shule hiyo ambayo iko jirani na hifadhi hiyo ilifungwa mwishoni mwa mwaka jana kutokana na matukio hayo hali ambayo ilisababisha wazazi kuogopa watoto wao kudhuriwa na wanyama hao hivyo kuwahamishia watoto wao kwenye shule ya Msingi ya Saadani.
Akizungumza jana, Mtendaji wa Kijiji cha Saadani, Hussein Msilu alisema mara baada ya matukio hayo wazazi wa watoto hao waliingia hofu na kuwaondoa watoto wao wapatao 67 na kuwahamishia kwenye shule hiyo ya Saadani ambayo iko umbali wa kilomita kati ya sita na saba.
Msilu alisema kutokana na hali hiyo uongozi wa kata na kamati ya shule kwa pamoja walikubaliana wanafunzi hao kuhamishiwa kwenye Shule ya Msingi Saadani kutokana na hofu iliyotanda kuwa wanafunzi wanaweza kuliwa na simba hao.
Alisema wanaushukuru uongozi wa kiwanda cha chumvi kwa kutoa usafiri kwa ajili ya kuwasafirisha wanafunzi kwenda na kurudi kutoka kwenye Kitongoji hicho cha Saadani Chumvi hadi shuleni Saadani, kwani umbali ulikuwa mrefu sana pia ni hatari kwani wanapita ndani ya hifadhi hiyo ambayo ina wanyama mbalimbali.
Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete alisema alipata taarifa hiyo na kuwasiliana na mamlaka husika na kwamba tayari zilichukuliwa za kuwaondoa simba hao, lakini kilichobaki kwa sasa ni hofu ya wananchi.
Aidha, aliwatoa hofu wazazi na kuwaambia wawarejeshe watoto hao shuleni hapo ili waendelee kusoma hapo kwani ni karibu na makazi yao tofauti na Saadani ambako ni mbali pia ni usumbufu mkubwa kwao, kwani hali hiyo imedhibitiwa.