WATU sita wamekufa na wengine 45 kujeruhiwa katika ajali mbili tofauti za barabarani zilizotokea juzi na jana mkoani Singida.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka alisema mjini hapa jana kuwa ajali ya kwanza ilitokea Juni 11 mwaka huu saa 1.30 usiku eneo la Manga nje kidogo ya mji huu kwenye Barabara Kuu ya Singida – Mwanza.
Alisema ajali hiyo ililihusisha basi lenye usajili wa namba T174 CAV Scania la Kampuni ya Nice Line linalomilikiwa na Enock Mwita wa jijini Mwanza ambalo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Mwanza.
Dereva wa basi hilo aliligonga kwa nyuma gari la mizigo lenye namba za usajili RAT 317N/ RL 0754 aina ya Benz lililokuwa limeegeshwa pembeni mwa barabara hiyo na kusababisha vifo vya abiria watatu papo hapo. Wengine wawili walifia hospitalini na kusababisha majeruhi 37.
Kwa mujibu wa Kamanda Sedoyeka, dereva huyo ambaye alikimbilia kusikojulikana baada ya ajali kutokea, alikuwa kwenye mwendo kasi. Katika ajali nyingine iliyotokea Juni 12 saa 12.15 asubuhi katika eneo la Kindai kwenye barabara kuu ya Singida – Dodoma nje kidogo ya mji huu, gari aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 998 CWG liliacha njia na kupinduka kisha kusababisha kifo cha abiria mmoja na majeruhi wanane.
Alisema abiria wa gari hilo walikuwa wakisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Kahama mkoani Shinyanga kwa ajili ya kuhudhuria mazikoi ya ndugu yao na gari lao lilipofika eneo la ajali kwenye kona kali dereva wake, Paul Bundala alishindwa kulimudu kutokana mwendo kasi.
Baadhi ya waliokufa katika ajali hiyo ni Shija Masanja,Yohana Chimole na Febronia Kway. Miili ya waliotajwa na wengine watatu ambao majina yao hayajatambuliwa imehifadhiwa katika hospitali ya mkoa wa Singida ambapo pia wamelazwa majeruhi.