Nimshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuamka nikiwa salama na kuandika haya nitakayoandika. Hakika ahimidiwe daima.
Wiki iliyopita nilisoma habari iliyomhusu Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambaye alimtolea uvivu mshauri wa zamani wa Siasa wa Rais Jakaya Kikwete, Kingunge Ngombale Mwiru kwa kuupinga mchakato wa uteuzi wa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kusema bila kupindapinda kuwa anakivuruga chama.
Mzee Kingunge aliyejitoa kufa na kupona kumpigania Mbunge wa Monduli na waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa, amekuwa akitoa matamko mbalimbali kuhusiana na mchakato wa kumpata mgombea urais na zaidi akisema haukutenda haki hasa baada ya kuenguliwa jina la Lowassa.
Kamati ya Usalama na Maadili, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, ndizo zilizokuwa na kazi ya kuchuja majina hadi kupatikana mgombea mmoja, Dk. John Pombe Magufuli.Makamba alisema: “Mzee Kingunge ni mtu mzima, ninamheshimu sana, ni mkongwe katika siasa, lakini anakivuruga chama.”
Alisema hakubaliani na kauli za Kingunge kupinga uteuzi wa Dk. Magufuli kwa sababu makada wote wa chama waliokuwepo Dodoma, waliamua kumpitisha kwa kuwa walimuona anafaa na anaweza kukijenga chama.
Makamba akaongeza: “Ndani ya chama kuna wazee wenye busara ambao waliangalia vitu vingi hadi kumteua mgombea kwani unaweza kuwa mtendaji mzuri lakini ukawa na kasoro nyingi hivyo, unaweza vilevile kuonekana ukashindwa kukivusha chama kwenye ushindi.
Licha ya maneno hayo ya kijana Makamba, mimi pia namheshimu sana Mzee Kingunge, lakini siwezi kukubaliana naye anavyokandia mchakato na niseme ukweli tu kwamba naye anakipasua chama na kama chama kingekuwa ni binadamu basi upasuaji huo ungekuwa unafanyika bila ganzi.
Mimi ninaamini mchakato ulikuwa sahihi, kila mgombea aliridhika (labda Lowassa) na ndiyo maana kura zilipigwa ndani ya Mkutano Mkuu wa CCM, chombo chenye maamuzi ya mwisho wajumbe wakiamini kuwa Dk. Magufuli anaweza kuongoza.
Dk. Magufuli nina imani kwamba atafanya vizuri kiuongozi hivyo ni bora apewe ushirikiano kama walivyopewa viongozi waliopita ili kuinusuru CCM na watu waendelee kukiheshimu kama awali.
Baba yake January Makamba ambaye ni katibu mkuu mstaafu wa chama hicho, Yusuf Makamba alitia ‘moto’ maneno ya mtoto wake alipokakaririwa na vyombo vya habari wiki iliyopita akisema kwamba, watu wanaoendelea kulalamikia mchakato wa kumpata mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Magufuli wana masilahi binafsi na siyo kwa ajili ya kukiimarisha chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake wiki iliyopita Mzee Kingune ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM alisema, Kamati ya Usalama na Maadili iliteka majukumu ya Kamati Kuu baada ya kuamua kuchuja majina ya makada waliojitokeza kuwania urais hadi kufikia watano, akisema jitihada hizo zilifanywa kwa kuvunja kanuni na zililenga kumuengua Lowassa kuwania kuingia ikulu.
Kingunge alisema kitendo cha kumuengua Lowassa kwa kuvunja kanuni kimeacha kasoro kubwa ndani ya chama hicho tawala kwa sababu taratibu zilikiukwa ili kupata viongozi.Alisema kosa hilo siyo la Dk. Magufuli aliyepitishwa kuwa mgombea urais wa CCM, na wala si la Lowassa, bali ni la waliopendekeza majina ya walioingia tano bora.
Jina la Lowassa, ambaye alijidhihirisha kukubalika ndani na nje ya CCM kutokana na harakati zake za kusaka wadhamini kujaa watu, halikupelekwa kwenye Kamati Kuu, kwa mujibu wa Kingunge na hivyo kutojadiliwa na chombo hicho ambacho kilimpitisha Dk. Magufuli, Dk. Asha-Rose Migiro, January Makamba, Bernard Membe na Balozi Amina Salum Ali.
Ninachoweza kusema ni kwamba Mzee Kingunge atafakari kama anachokifanya sasa ni cha kujenga chama? Je, semasema yake nje ya vikao vya chama, atasikilizwa na wenzake? Je, kwa nini vigogo hao wamuengue Lowassa?
Mimi naamini walikuwa na sababu nzito ambazo bila shaka kuzisema zingeweza kuvuruga chama, hivyo busara na hekima zilitangulizwa.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.