Mpango wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumtangaza kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Edward Lowassa, kujiunga na chama hicho uliotarajiwa kutekelezwa jana, umekwama huku kukiwa na taarifa za mgawanyiko ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wiki iliyopita, Mtandao huu uliandika taarifa kwamba Chadema walipanga kumtangaza Lowassa Jumapili ya jana baada ya kumaliza mazungumzo naye, lakini hilo lilishindikana.
Taarifa kutoka ndani ya Chadema zinadai kuwa huenda kada huyo ambaye mustakabali wake ndani ya CCM uliingia dosari baada ya jina lake kuondolewa alipokuwa akisaka urais, sasa huenda akatangazwa rasmi wakati wowote wiki hii.
“Kwamba anakuja Chadema hiyo si siri tena, lakini ule mpango wa kumtangaza leo (jana) haukufanikiwa kutokana na kuwapo kwa vikao tofauti muhimu vya vyama viwili ndani ya Ukawa, Chadema na CUF,” alisema mtoa habari wetu ndani ya Chadema.
Jana, Chadema waliitisha mkutano wa dharura wa Kamati Kuu jijini Dar es Salaam wakati ambapo CUF nao walikuwa na mkutano wa Baraza Kuu huko Zanzibar, wote wakijadiliana suala moja tu; urais ndani ya Ukawa.
Vikao hivyo vilivyogubikwa na usiri mkubwa vilitarajiwa kumalizika jana mchana na kisha jioni wenyeviti wenza wa Ukawa walipanga kuzungumza na wahariri wa vyombo vya habari, lakini mkutano huo uliahirishwa kutokana na kushindwa kumalizika kwa wakati vikao hivyo nyeti.
Akizungumza na mtandao huu jana, Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Abdul Kambaya, alisema kwa ufupi kuwa kilichokuwa kikijadiliwa na chama hicho kitawekwa hadharani leo, huku Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed naye akisema: “Tutawafahamisha kinachozungumzwa baada ya kikao kumalizika.”
Watu wa karibu na CUF wanadai kuwa uongozi wa juu wa chama hicho, hasa Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba, hadi jana hakuwa akiafiki ujio wa Lowassa Ukawa.
“Sijui itakuwaje lakini kama msimamo wa Profesa ukiendelea hivi, sioni namna gani CUF itaendelea kuwamo ndani ya Ukawa. Kwanza kura ambazo huwa anazipata kwenye urais nazo ni muhimu sana kwani husaidia chama kupata ruzuku.
“Sasa iwapo hatagombea na labda akagombea Lowassa kupitia Chadema ndani ya Ukawa, basi suala la ruzuku litaleta balaa kwani ndizo fedha zinazosaidia kuendesha ofisi za CUF Tanzania Bara,” alisema mwanachama mmoja wa CUF, akizungumzia utata uliokigubika chama hicho unaohatarisha maisha ya Ukawa kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
Kwa upande wa Chadema, mtandao huu ulihakikishiwa jana kuwa wao hawana shaka na ujio wa Lowassa, wakiandaa mazingira ya kumsafisha mbele ya wananchi kwa madai kuwa kilichofanya aonekane mchafu ni mfumo ndani ya CCM na wala si yeye kama Lowassa.
Ingawa kumekuwapo madai kuwa wanafamilia ya Lowassa na marafiki zake wachache wamekuwa wakimshauri kutohama CCM, lakini Lowassa ndiye mwenye uamuzi wa mwisho na kwamba mmoja wa rafiki zake wakubwa na mfanyabiashara maarufu nchini amewahi kusikika akikiri kuwa ameshindwa kumshawishi rafiki yake huyo kubaki CCM.
LOWASSA Atua Rasmi CHADEMA.......Kutangazwa Muda Wowote Ndani ya Wiki Hii
0
July 27, 2015
Tags