CHARLES Makongoro Nyerere (CMN) ni miongoni mwa wanachama wa CCM waliotangaza nia ya kutaka kuchaguliwa kuwania urais kupitia chama hicho mwaka huu. Raia Mwema lilifanya naye mahojiano wiki hii nyumbani kwake jijini Dar es Salaam. Endelea
-RAIA MWEMA: Kwanini wana CCM wanatakiwa wakuchague wewe uwe mgombea wao na si mwingine miongoni mwa wenzako 41 waliojitokeza kuwania nafasi hiyo?
MAKONGORO: Mimi si mwizi, wala mla rushwa. Nina uzoefu wa kutosha na nakijua chama changu. Pia ni mtu ambaye napenda kufuata utaratibu. CCM sasa inahitaji mtu wa namna hiyo.
-RAIA MWEMA: Kwanini unadhani uadilifu ndiyo sifa kuu ya Rais ajaye wa Tanzania?
MAKONGORO: Naamini kuwa ni mtu mwadilifu pekee ndiye ambaye ataisaidia nchi yetu kuondokana na matatizo tuliyonayo. Ufisadi, wizi wa mali ya umma na matatizo yote tuliyonayo yataondoka endapo tutampata kiongozi ambaye ni muadilifu.
Kinachotakiwa ni kwa chama kujisafisha chenyewe kwanza. CCM ikiwa safi, serikali itakuwa safi tu. Lakini serikali haiwezi kuacha kuwa ya kifisadi wakati chama chetu kina mafisadi na tunawavumilia.
-RAIA MWEMA: Ina maana kama utafanikiwa kuwa Rais na hatimaye Mwenyekiti wa CCM unaweza kuwafukuza wanachama wote wenye tuhuma za ufisadi?
MAKONGORO: Hapana, siwezi kumfukuza mwanachama kutoka CCM. Tunachoweza kufanya ni kuwatoa kutoka katika nafasi zao za uongozi. Nitakupa mifano miwili kueleza hili.
Kwa mfano wewe ni Mwislamu. Dini yako inataka uwe unaswali swala tano kwa siku. Sasa pale msikitini kwako una Imamu ambaye kwa siku anahudhuria swala moja au asihudhurie kabisa. Lakini kila siku unaambiwa anaonekana klabu ya pombe akinywa.
Sasa huyu imamu dawa yake si kumvua Uislamu wake. Unachofanya ni kumtoa kwenye uimamu na kumpa mtu mwingine ambaye hatawakwaza.
Kama wewe ni Mkristo na una Paroko ambaye kila kukicha ana kashfa za ngono na wake za watu ingawa hajawahi kukutwa huyo si paroko. Sasa ikitokea siku akanusurika kufumaniwa hadi akaacha mavazi yake ya uparoko kule Guest House lakini akachoropoka bila kukamatwa; huyo humvui Ukristo wake. Unachofanya ni kumtoa kwenye Uparoko wake.
Chama ni imani kama zilivyo dini. Huwezi kumwondoa mtu kwenye chama lakini unaweza kumwondoa kwenye nafasi za uongozi. Kwa kifupi, kuna maparoko na maimamu wa aina hiyo ndani ya CCM ambao ni lazima kuwaondoa kwenye nafasi zao kama kweli tunaitakia mema nchi yetu.
-RAIA MWEMA: Unasema chama ni imani lakini wewe uliondoka CCM na kuhamia NCCR Mageuzi kwenye miaka ya 1990. Ilikuaje ukahama chama chako?
MAKONGORO: Mojawapo ya matatizo ya chama chetu ambayo ni lazima Rais ajaye apambane nayo ni ukweli kwamba kuna majimbo ya uchaguzi hapa Tanzania ambayo kama mtu hutoi rushwa huwezi kupita.
Arusha ni mojawapo ya maeneo hayo. Yaani kama hula hela sahau kuhusu kuchaguliwa. Utafanyiwa mizengwe na viongozi wala rushwa hadi mwenyewe utachoka na kukata tamaa.
Mimi mwaka ule wa 1995 nilikumbwa na tatizo hilo. Nilitaka ubunge pale Arusha lakini mtandao wa rushwa ulikuwa ukiniwekea vikwazo. Sasa wazee wawili wa pale; mmoja amefariki dunia na mwingine yuko hai, wakanishauri kuwa kwa vile wananchi wananitaka na shida yao ni kiongozi mzuri, nihamie kwenye chama kingine. Ndiyo nikaenda NCCR Mageuzi na nikapata ubunge.
Haya ndiyo mambo ambayo yamenifanya niingie kwenye kinyang’anyiro kwa sababu hali inazidi kuwa mbaya. Kama hali ikiachwa hivi basi hata kwenye urais atakayeshinda atakuwa ni mla rushwa tu na nchi itakwenda vibaya sana.
-RAIA MWEMA: Kuna taarifa kwamba Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, aliwahi kutaka kukuteua kuwa mbunge wakati akiwa Rais lakini wewe ulikataa. Kuna ukweli gani katika hili?
MAKONGORO: Katika watu ambao nawaheshimu sana kama viongozi hapa nchini, Mzee Mkapa ni mmoja wao. Aliikuta nchi ikiwa na hali mbaya sana lakini akaicha pazuri. Aliikuta inanuka madeni lakini akaondoka akiiacha na akiba kubwa ya fedha za kigeni.
Sasa miezi 18 kabla hajamaliza urais wake, aliniambia anataka kuniteua kuwa mbunge. Ni kweli kuwa nilikataa nafasi hiyo. Nilikataa kwa sababu ingeonekana anampendelea mtoto wa Nyerere. Ingeonekana kama anatoa zawadi. Na pengine ingeweza kujenga picha kuwa nimebebwa.
Nilikataa kwa sababu sikutaka mtu ambaye ninamuheshimu sana anyooshewe vidole kwa ajili yangu. Nilimueleza sababu zangu na nashukuru mzee yule alinielewa vizuri.
-RAIA MWEMA: Ni kweli kwamba baba yako, Mwalimu Julius Nyerere, hakujua kwamba uko vitani Uganda wakati wa Vita ya Kagera hadi baada ya vita kumalizika?
MAKONGORO: Ni kweli. Unajua mimi nilikwenda vitani nikiwa na umri wa miaka 18 tu ambao ndiyo ulikuwa umri mdogo zaidi kuruhusiwa kwenda vitani wakati huo.
Wakati vita inaanza mimi nilikuwa kwenye mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwenye Operesheni iliyojulikana kama Chakaza. Wale waliokuwa JKT walipatiwa mafunzo kidogo na kisha kupelekwa vitani.
Mimi pia nikaenda lakini sikumwambia baba. Ulikuwa ni uamuzi wangu binafsi. Kuna kaka zangu walikuwa jeshini tayari wakati huo lakini mimi nilikuwa mdogo sana.
Baba alikuwa na mambo mengi ya kufanya wakati wa vita na nadhani alijua naendelea na JKT. Kwa bahati nzuri pale nyumbani Msasani kulikuwa na simu na baada ya vita askari tulikuwa tukirusiwa kupiga simu nyumbani.
Sasa nikaanza utaratibu wa kupiga simu nyumbani mara kwa mara kila ilipofika saa kumi jioni. Baba alikuwa na utaratibu wa kurudi nyumbani saa tisa na akirudi moja kwa moja anakwenda mezani ale chakula.
Baada ya muda akabaini kuwa kila saa kumi wadogo zangu wakisikia tu simu wanakimbilia ilipo kwenda kusikiliza. Siku moja akawauliza, mbona mnakimbilia simu kila inapofika saa kumi na saa nyingine hamkimbilii?
Ndiyo wakamwambia tunaongea na kaka Mako (Makongoro). Akashangaa, akawaambia mnaongea naye kutoka wapi? Wakamwambia yuko Uganda. Nalisikia alishtuka sana na moja kwa moja akaja kwenye simu.
Mara nikasikia sauti ya Mwalimu ikiuliza Uko wapi Makongoro? Nikamwambia niko vitani Uganda? Akaniuliza uliendajeendaje? Nikamuuliza kwani vijana wenzangu kama mimi waliendajeendaje?
Basi, nikasikia anapumua na akaanza kuniuliza kuhusu habari za Uganda na mambo mengine. Nilikuwa sijawasiliana na baba yangu kwa muda wa miaka miwili tangu kuanza kwa vita.
-RAIA MWEMA: Mmoja wa washindani wako kwenye kinyang’anyiro hiki cha kuwania urais, Edward Lowassa, amewahi kuhadithia namna alivyoshuhudia watu wakifa vitani wakati wa vita hiyo. Je, mliwahi kukutana mkiwa Uganda?
MAKONGORO: Sikumbuki kukutana na Lowassa wakati wa Vita ya Uganda. Lakini kulikuwa na askari wengi na inawezekana nilipokuwa mimi yeye hakuwepo. Siwezi kujua askari wote waliopigana vita ile.
Baada ya vita kumalizika, wasanii wengi kama vile Zahir Ally Zorro walikuja Uganda kututumbuiza lakini Lowassa pia sikumuona. Nasikia yeye alisomea sanaa Chuo Kikuu labda alikuja wakati huo lakini pia sikumuona.
Zorro na marehemu Kapteni John Komba niliwaona wakati ule. Lakini Lowassa sikumbuki kumuona. Labda alipigana mji mwingine au alikuja na wasanii kutumbuiza baada ya vita, lakini mimi sikumbuki kumuona.
-RAIA MWEMA: Washindani wako wanadai kuwa wewe hufai kupewa urais kwa sababu ni mlevi na unapenda kunywa pombe. Unazungumziaje shutuma hizi?
MAKONGORO: Mimi pombe nakunywa lakini hilo la kusema kwamba mimi ni mlevi halipo. Mimi si mlevi. Wapo wapinzani wangu ambao ni walevi kiasi kwamba pombe zimeharibu afya zao na sasa wanaumwa.
Wanaumwa kwa sababu ya kunywa pombe. Mimi kama unavyoniona niko fiti na sina tatizo lolote la kiafya. Sasa wale ambao ulevi umewasababishia matatizo hawasemwi na kibao kinageuzwa kwangu. Hiki ni kichekesho kwelikweli.
-RAIA MWEMA: Kwa hiyo uko tayari kwenda kupimwa afya ili uthibitishe utimamu wa afya yako kama alivyopendekeza mgombea mmoja kwamba wagombea wote mpimwe afya zenu?
MAKONGORO: Tupimwe afya kwani tunataka kwenda kuchezea Real Madrid au Manchester United? Wachezaji wanaotaka kwenda kucheza mpira ndiyo wanapimwa afya zao lakini sijasikia popote watu wanaotaka urais wanaenda kupima afya.
Kwani Watanzania hawawezi kuangalia tu wenyewe na wakajua huyu ana afya njema na yule hana?
-RAIA MWEMA: Una wito gani kwa wana CCM wenzako kuelekea kuchagua mgombea urais kupitia chama chenu kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu?
MAKONGORO: Mimi nasema wana CCM wanatakiwa watutendee haki wagombea, chama chao na taifa lao. Kwenye uchaguzi huu, CCM inaweza kuamua kufanya mabadiliko chanya au hasi.
Wakichagua mtu ambaye dunia nzima inajua ni mwizi, wajue kwamba Watanzania watawaona na dunia pia itawaona pia.
Wana CCM wasibabaike na kauli za vitisho zinazotolewa na baadhi ya wagombea kwamba wasipopitishwa wao, basi patachimbika.
Sasa nauliza, patachimbika kwani kuna madini gani yanayotafutwa? CCM imekuwa Mererani ambako wachimba madini wanachimba kutafuta Tanzanite?
Kama wana CCM watafanya makosa safari hii, wajue kwamba hawakuwa na wa kumlilia isipokuwa wao wenyewe.
Chanzo: Raia Mwema
Makongoro: Lowassa sikumuona Vita ya Kagera, Labda alikuja baada ya vita kuburudisha wanajeshi
0
July 02, 2015