WAKATI Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, akipangua ratiba ya vikao muhimu vya Kamati ya Usalama na Maadili pamoja na Kamati Kuu vilivyotarajiwa kufavyika juzi na jana, Mwanasiasa maarufu, Kingunge Kombale-mwiru jana alikuwa uso kwa uso na Katibu Mkuu wa chama hicho katika jitihada za kumuokoa Edward Lowassa.
Katika siku ya jana kulikuwe na minong’ono ya hapa na pale iliyokuwa imeenea katika korido za Makao Makuu ya CCM na viunga vya mji wa Dodoma, ikidai kuwa jina la mwanasiasa huyo halitakuwemo katika orodha ya majina ya tano bora itakayopelekwa ndani ya NEC kutoka Kamati Kuu.
Minong’ono hiyo ya kuwepo uwezekano wa jina la Lowassa kutotoka Kamati Kuu, iliongeza hofu zaidi miongoni mwa wapambe wa mwanasiasa huyo, baada ya mwanasiasa mkongwe nchini anayejulikana wazi kuwa katika kambi ya mgombea huyo, Kingunge Ngombale-Mwiru kutinga katika Ofisi za Makao Makuu ya chama hicho mchana wa kati ya saa 8:00 na saa 9:00.
Baada ya kushuka kwenye gari lake na kuelekea moja kwa moja katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM, Kingunge alisikika akisema “Nina miadi ya kuonana na Katibu Mkuu saa 8.30 mchana huu, ameniita.”
Mwanasiasa huyo ilimchukua takriban saa nzima akiwa katika ofisi ya Kinana. Alipotoka tu nje, kada mwingine wa CCM, Hamis Mgeja, ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Shinyanga aliingia katika ofisi ya Kinana akidaiwa kuitwa pia.
Mgeja, kama ilivyo kwa Kingunge, ni miongoni mwa makada wa CCM ambao wamekuwa wakijipambanua wazi wazi kuwa katika kambi ya Lowassa kiasi cha makada hao kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mgombea huyo wa kutafuta wadhamini 450 katika mikoa 15 ya Tanzania, kati ya hiyo mitatu ikiwa ni ya Zanzibar.
Haikuweza kufahamika kwa undani ni kwanini makada hao wa CCM waliitwa na Kinana ofisini kwake, lakini baadhi ya wadadisi wa mambo walielezea tukio hilo kama sehemu ya juhudi za kambi hiyo ya Lowassa kuokoa jahazi la mgombea wao huyo jina lake kuondolewa mapema na Kamati Kuu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ratiba ya awali ya mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, vikao hivyo muhimu katika mchakato huo vilitarajiwa kufanyika juzi na jana, lakini vikao vyote viwili hivyo havikuweza kufanyika kama vilivyopangwa, huku kukiwa hakuna taarifa yoyote rasmi kwanini havikufanyika.
Kwa kawaida kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili ambacho huongozwa na Rais Kikwete mwenyewe akisaidiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahiman Kinana, ndicho kinachotoa dira ya mwelekeo kwa wajumbe wa Kamati Kuu, kikao ambacho kina mamlaka ya kuteua majina matano kutoka miongoni mwa wote waliojitokeza kuomba nafasi hiyo.
Kikao hicho cha Kamati ya Usalama na Maadili ndicho kinachopokea majina ya wote waliojitokeza kuomba nafasi hiyo, kabla ya kujadili mienendo ya kimaisha ya kila mmoja wa wagombea, hasa katika suala zima la kimaadili na uzingatiaji wa miiko na viapo vya utii kwa chama hicho.
Baada ya Kamati hiyo kukamilisha kazi hiyo, majina yote ya walioomba uteuzi huo huwasilishwa ndani ya kikao cha Kamati Kuu, kila jina likiwa limetendewa haki kwa kubeba maelezo ya sifa za miendendo hiyo ya kiamaadili na uzingatiaji huo wa miiko na viapo vya utii kwa Chama, kabla ya kikao hicho kuteua majina matano yanayopelekwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) kwa hatua zaidi.
Kutofanyika kwa vikao hivyo muhimu katika mchakato huo wa uteuzi ndani ya CCM hadi jana kama ilivyokuwa imepangwa awali, kwa kiasi fulani kumeongeza hofu na kukoroga vichwa vya baadhi ya wapambe wa wagombea wa urais kutokana na kutofahamu sababu na malengo ya kuahirishwa huko kwa vikao hivyo.
Hadi jana jioni ya Julai 9, 2015, vikao hivyo muhimu viwili vinavyoongozwa na Rais Kikwete mwenyewe, havikuwa vimefanyika kutokana na kile kilichoelezwa na watu wa karibu na kiongozi huyo mkuu wa nchi na chama chake hicho kwamba ni kukabiliwa na majukumu mengine mazito ya kitaifa.
Kwa siku ya jana Alhamisi pekee, Rais Kikwete alikuwa na jukumu la kuzindua ukumbi wa kisasa wa Mkutano Mkuu wa CCM uliojengwa kwa gharama za chama hicho katika eneo lililopo karibu na majengo ya Ofisi za Hazina Ndogo mjini Dodoma, hafla iliyofanyika kuanzia asubuhi hadi mchana kabla ya alasiri kiongozi huyo kwenda kulihutubia Bunge na kufunga shughuli za Bunge la Bajeti.
Katika korido na viunga vya Ofisi za Makao Makuu ya CCM pamoja na maeneo ya Dodoma Hotel na NAM Hotel ambako wengi wa wapambe hao wa Lowassa wamechukua vyumba kwa ajili ya malazi, wengi wao walikuwa wakionyesha nyuso za huzuni, huku wakionekana kuchanganyikiwa bila kufahamu ni nini hasa kilichokuwa kikiendelea ndani ya chama hicho.
Moshi Mweusi Watanda CCM.......Rais Kikwete Apangua Ratiba ya Vikao vya Kamati ya Maadili na Kamati Kuu, Kingunge Amvaa Kinana
0
July 10, 2015
Tags